SERIKALI kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeongeza idadi ya wanyamapori katika hifadhi ndogo ya asili ya Luhira iliyopo katikati ya Mji wa Songea mkoani Ruvuma.
Akizungumza baada ya kuwafikisha salama wanyama hao
kwenye hifadhi ya Luhira, Mhifadhi Mkuu wa Wanyamapori wa TAWA, Asharaf Shemoka
amewataja wanyamapori walioletwa katika hifadhi hiyo ni nyumbu watatu kati yao
dume mmoja na pofu watatu kati yao dume mmoja.
Amesema wanyamapori hao wametolewa katika Shamba la ufugaji wanyamapori Majichai
Halmashauri ya Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha na kwamba wanyama hao licha ya
kusafiri umbali mrefu wamefika Songea wakiwa na hali nzuri.
Hata hivyo,amesema huo ni mpango wa awali wa kuleta
wanyamapori katika hifadhi ya Luhira na kwamba wanatarajia kuongeza wanyama
zaidi wakiwemo mbuzi mawe, kongoni, swalapala na wanyama wengine kadiri
itakavyowezekana.

Baadhi ya wanyamapori ambao wameongezwa hifadhi ndogo ya asili Luhira mjini Songea na wanyamapori ambao wapo katika hifadhi hiyo iliyopo katikati ya mji wa Songea
“Hifadhi ya Luhira ina eneo kubwa, ambalo linahitaji
uwekezaji mkubwa,tunafikiria kuwaleta wanyama wakubwa kama twiga na simba ambao
watawekwa kwenye uzio maalum(cage)’’,alisisitiza Shemoka.
Hata hivyo amesema katika awamu ya kwanza
wamedhamiria kuwaleta wanyamapori 26 na kwamba wataendelea kuwaleta kadri
malisho yatakavyokuwa yakiongezeka na kwamba wataanzisha bustani ndogo ndogo za
wanyama ndani ya hifadhi ya Luhira.
Naye Mkuu wa Kikosi Dhidi ya Ujangili Kanda ya
Kusini(KDU) ambaye pia ndiyo Msimamizi Mkuu wa Hifadhi ya Luhira Keneth Sanga
amesema baada ya kuongeza idadi ya wanyamapori sasa wanatarajia pia idadi ya
watalii itaongezeka.
Anatoa rai
kwa wakazi wa Mkoa wa Ruvuma na mikoa ya kusini kufika katika hifadhi ya Luhira
kujionea fursa za utalii zilizopo katika hifadhi hiyo pekee ya asili nchini Tanzania iliyopo mjini
Songea.
Hata hivyo amesema idadi ya wanyamapori wanaokula
nyasa kwenye hifadhi hiyo wameongezeka
ambapo hivi kuna pundamilia,pofu,nyumbu,swala,ngolombwe,swalapala na wanyamapori
wengine.
Hifadhi
ndogo ya asili Luhira yenye ukubwa wa hekta 600 ilianzishwa mwaka 1974,ipo umbali wa kilometa
saba kutoka mjini Songea.
Mhifadhi
wa TAWA katika Hifadhi ya Luhira David Tesha amewataja wanyama wengine ambao
wanapatikana katika hifadhi hii ni fisimaji, nyani,pongo,tumbili, kakakuona, na
kobe,pia bustani hiyo ni makazi ya reptilia na ndege wa aina mbalimbali.
Tesha
amesema hifadhi ya Luhira ni eneo la
asili lenye utajiri wa miti ya miyombo, misuku, mitumbitumbi, miwanga, minyonyo,mizambarau,mininga,
na mikuyu,na kwamba ni miongoni mwa bustani chache zenye uoto wa asili kabisa
zilizopo mjini.
Amesema
ndani ya Luhira,mtalii anaweza kufanya utalii wa kutembea kwa miguu,kupiga
picha,kuangalia wanyama na ndege,utalii wa kuweka kambi(camping) na kufanya
mapumziko ya mchana(picnic) hufanyika ndani ya eneo maalum.
“Watalii
kutoka nje ya nchi pia wanatembelea hifadhi yetu, tumepokea watalii toka
Ujerumani,Afrika ya Kusini, India, Marekani, Ufaransa, Italia, Uholanzi na wageni
toka mikoa mbalimbali nchini, wanafanya utalii wa kuchunguza aina ya mimea na
ndege’’, alisema Tesha.
Hifadhi
ya asili ya Ruhila,inafikika kwa urahisi kwa ndege au kutumia barabara ya
Njombe hadi Songea,Mtwara hadi Songea ambayo ni ya lami,ukifika Songea mjini eneo
la Msamala unasafiri kwa barabara kilometa 3.5 unatakuwa umefika bustani ya
Luhira.
Malazi
ya wageni yanapatikana Manispaa ya Songea ambapo wageni pia wanaweza kuweka
mahema ya muda katika maeneo yaliyotengwa ndani ya hifadhi hiyo.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Juni 27,2021
Comments
Post a Comment