UMUHIMU WA UTALII WA NDANI KWA WATANZANIA

 

 


Na Rhoda Simba, Dodoma.

Mara nyigi jamii imezoea kuona kwamba kitendo cha kufanya utalii ni  utamaduni wa watu wa nje huku  wengine wakifiria  kuwa unawahusu watu wenye kipato cha juu .

Ukweli ni kwamba mtu anaweza kutoka na marafiki siku za mwishoni mwa juma na kwenda kufurahia na marafiki, akatumia kiasi kikubwa cha fedha lakini linapokuja suala la kwenda kufanya utalii linaonekana kama anakwenda kupoteza fedha nyingi sisizo na msingi.

Tunapo zungumzia Utalii ni kile kitendo cha kusafiri kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine kwa lengo la kuburudika, kujifunza au makusudi mengine.

Kufuatia suala la utalii wa ndani kuendelea kuzorota katika nchi nyingi za Afrika,baadhi ya Asasi binafsi na makampuni ya Utalii Tanzania,yameanza kutafuta mikakati ambayo itasaidia kuamsha ari ya raia kutembelea vivutio vyao na kuachana na dhana kudhani kuwa utalii ni kwaajili ya wanaotoka nchi za Ulaya tu.

Kwa miaka mingi tumekuwa hatuna utaratibu wa kutembelea vivutio kwenye maeneo mbali mbali kama vile hifadhi, sehemu za kihistoria, makumbusho, na sehemu nyingine zinazovutia.

Mara nyingi watu wengi wanaposikia masuala ya utalii, huwa wanajitoa kabisa na kuona kuwa hawastahili kuwa kwenye kundi la watalii, wanaamini watalii ni wazungu tu.

Wengine wanafanya hivyo kwa kuwa hawajaona faida za kuwa watalii, hawaoni faida za kutembelea maeneo yenye vivutio mbali mbali hapa nchini.

FURSA

Fursa zipo kila mahali, ila unahitaji macho tu kuziona, lakini kuna njia nyepesi sana inayotumiwa na watu wengi waliofanikiwa kujua fursa ipo wapi, njia hiyo ni kwa kutembelea sehemu hizo, watu wengi wanao fanyabiashara wameona fursa kwa kuwa maeneo ambayo ni tofauti na maeneo waliyozoea.

Kwa kutembelea hifadhi na vivutio mbali mbali hapa Tanzania utajionea fursa nyingi sana za uwekezaji, biashara, kilimo, ufugaji na nk. Fursa ambazo huwezi kuziona kwa kukaa tu sehemu moja maisha yako yote. Amka hapo ulipo nenda nje ya eneo ulilopo.

Usiogope gharama kwasababu ni muhimu sana kwako kusafiri, jipe nafasi ya kuona mambo mapya kabisa ambayo akili yako haijawahi kuyaona Pia hizi ni sehemu nzuri kwa kuangalia masoko ya bidhaa zako ulizonazo.

USHIRIKIANO KWENYE MASUALA YA UHIFADHI WA WANAYAMA PORI NA RASILIMALI.

Naamini watu wanapotembelea maeneo ya mbuga za wanyama, au vivutio vingine watapata na muda wa kupata maarifa na watu wanaofanya kazi kwenye maeneo hayo, wata elezea mafanikio, jinsi wanavyofanya kazi, wataelezea na changamoto wanazokutana nazo wakiwa kazini.

Kwa mfano ikiwa watu watatembelea hifadhi za wanyama wataelezwa changamoto kubwa ya kukosa wageni, ujangili na kukosa wataalamu wa fani fulani. 

Hivyo kwa watu kupata taarifa za namna hii wanaweza kusaidia kwa kutoa ushirikiano na msaada mbali mbali yenye lengo la kuhifadhi maliasili zetu, misaada hivyo inaweza kuwa ya mawazo, au ya kifedha hivyo ni muhimu tukawa na utaratibu wa kutembelea vivutio vyetu.

 

NJIA BORA YA KUTANGAZA UTALII WA NDANI.

Watu wanapokuwa na utamaduni mzuri wa kutembelea maeneo yenye vivutio mbali mbali ndani ya nchi yetu, ndio huwa watangazaji wazuri wa utalii wetu.

Ikiwa tunahitaji  vivutio vyetu vijulikane kila mahali tunapaswa kuwa na utamaduni wa kutembelea vivutio. 

kila Mtanzania kuwa balozi mzuri kwenye kuutangaza utalii wetu ni kwa njia ya kutembelea hifadhi na maeneo ya vivutio. Mimi naamini sana katika hili na ni njia ya gharama nafuu sana kuutangaza utalii na vivutio vyetu.

 

KUINUA UCHUMI NA KUHARAKISHA MAENDELEO.

Watu wanapokuwa na utamaduni wa kutembelea vivituo wanakuwa ndiyo wachangiaji wakuu wa ukuaji wa uchumi kwa kuongeza mapato ya ndani Kupitia utalii .

Kwa kiingilio ambacho watatoa kwenda hifadhini au maeneo ya vivutio itasaidia sana kuinua uchumi wa nchi yetu ni njia nzuri sana ya kuanzia ili tuitoe nchi yetu kwenye utegemezi mkubwa wa misaada ya kifedha kutoka kwa mataifa mengine tukiwa na utamaduni wa namna hii wa kutembelea hifadhi na vivutio mara kwa mara, tutaipeleka nchi yetu mbali  kiuchumi.

Naamini umepata mwanga na sababu za msingi kabisa za kutembelea maeneo ya vivutio, kuna sababu nyingi lakini hizo saba zitufikirishe Usisahau kumshirikisha mwingine makala hii. Jijengee utaratibu huu, ni mzuri sana utaimarisha afya ya akili na afya ya mwili na roho yako pia.

Hapa tunakutana na Shirika la hifadhi za Taifa TANAPA ambapo shirika hili limepewa dhamana ya kusimamia ,kuendeleza maeneo yalioanzishwa kisheria kuwa hifadhi za taifa .

Maeneo hayo yanawakilisha kiwango cha juu kabisa cha uhifadhi wa wanyama pori, ambapo kwa wakati huu shirika linasimamia hifadhi 22 eneo linalosimamiwa na hifadhi ya taifa ni takribani kilometa za mraba 404,464 sawa na asilimia 11 ya eneo.

MADHUMUNI

Madhumuni ya Shirika la Hifadhi ya Taifa TANAPA ni kuhifadhi maeneo yaliyo na thamani/sifa za kipekee zinazoonesha urithi wa mali za kiutamaduni au maliasili za taifa .

Paia kuhifadhi maeneo yenye mifumo bayana ya aina maalumu za maliasili na kuhifadhi vyanzo vya maji na ardhi ambavyo ni muhimu katika kudumisha uwianao na kiikolojia na ambayo vinachangia mahitaji ya kujikimu ya watu waishio karibu na mipaka ya hifadhi na taifa kwa ujumla.

Madhumuni mengine ni kuhifadhi maeneo yanayotoa fursa kwa umma kwa ajili ya manufaa yao kimaisha,kiburudani na taiti za kisayansi.

Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Dodoma Ahamed Mbugi kutoka  TANAPA  amewataka wanahabari  kutumia kalamu zao katika kutangaza utalii wa ndani.

Kamishna Mwandamizi wa Uhifadhi Dodoma Ahmed


“Kumekuwepo na tabia ya jamii kuamini kuwa kutalii ni mpaka lazima utoke nje ya nchi wakati kuna maeneo mengi ya kufanya utalii ndani ya nchi ambayo hawayafahamu wala kuyatembelea,”

Na kuongeza kusema kuwa “lazima tujenge utamaduni wa kutembelea vivutio vyetu vya ndani zipo nchi ambazo watalii wengi ni wakazi wan chi husika  mfano nchi ya Afrika kusini watalii wengi ni wakazi wan chi hiyo na wamekuwa wakienda muda wote  kutembelea hifadhi na maeneo mbalimbali ya kitalii katika nchi yao,” amesema Kamishina Mbugi

Pascal Shelutete ni kamishina Uhifadhi Msaidizi Mwandamizi wa Mawalisiano wa TANAPA anaeleza kwamba  kwasababu watanzania jamii muamko bado ni mdogo wameanda mpango mkakati wakuboresha na kuendelea kutangaz vivutio vya kitalii kupitia Televisheni ikiwemo Tanzania safari Channel,Channel ya shirika la utangazaji Tanzania TBC ,vipindi vya radio na mitandao ya kijamii.

Kamishina Uhifadhi Msaidizi Mwandamizi TANAPA Pascal Shelutete


Anabainisha shirika linatoa fursa kwa sekta binafsi katika kuendeleza na kukuiza utalii katika hifadhi za taifa kwa kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi na umma ili kuwekeza katika meneo ya hifadhi.

Naye  Ofisa uhifadhi Mkuu wa shirika hilo July Lyimo amesema utalii husaidia kukuza uchumi na pato la taifa,kuongeza ajira , nakuitambulisha nchi kwa ujumla.

“Niwaombe waandishi wa habari mtumie kalamu zenu katika kuhakikisha tunawaelimisha ,hamasisha watanzania kuona umuhimu wa kwenda kutembelea Hifadhi za Taifa,”amesema July.

Mwisho.

 

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.