WATANZANIA WASHAURIWA KUTEMBELEA VIVUTIO VYA NDANI VYA UTALII

Na. Mwandishi Wetu, MWANZA

 

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja amesisitiza kuwa fursa zilizoko kwenye Sekta ya Maliasili na Utalii zikitumika ipasavyo zitasaidia kukuza pato la Taifa na uchumi wa mtu mmoja mmoja.

 


Mhe. Mary Masanja ametoa Kauli hiyo leo jijini Mwanza wakati wa  kikao cha pili cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Mwanza kwa Mwaka 2020/2021. Amesema takwimu za watalii wanaoingia hapa nchini kuanzia mwaka 1993 walikuwa 230,000. Aidha, mwaka 2019 idadi hiyo ya watalii iliongezeka na kufikia milioni 1.5.

 

"Idadi ya Watanzania kwa sasa ni milioni 60, lakini ukingalia takwimu hizo watalii wanaoingia kwenye hifadhi zetu kuangalia vivutio ni milioni 1.5, hii inaonesha sisi Watanzania tuna kazi kubwa ya kufanya, kuwa wazalendo na kupenda vile tulivyo navyo" amesema Mhe. Masanja.

 

Katika hatua nyingine, Mhe. Mary Masanja amewaeleza viongozi wa mkoa huo  kuwa uwepo wa vivutio vingi vya Utalii katika Kanda ya ziwa ni fursa pekee ya wananchi kuendelea kunufaika akitoa wito kwa viongozi waliohudhuria mkutano huo  wahamasishe Utalii wa ndani kwa nguvu zote.  "Ni lazima tuongeze nguvu katika kuhamasisha utalii  wa ndani bila kusahau kuhamasisha wageni kutoka nje ya nchi yetu , Utalii wa ndani unatuhusu sisi wenyewe ,nikiuliza hapa wangapi wamefika kwenye hifadhi zetu na kwenye vivutio  mbalimbali tulivyonavyo tutabaini  idadi kidogo sana, nawaomba sana tuhamasishane ’ amesisitiza Mhe. Mary Masanja.

 

Ameongeza kuwa janga la Corona limesababisha  kuyumba kwa sekta Utalii duniani kote pia hapa nchini  kwa kuwa watalii  waliokua wakitegemewa nchi zao zimeathiriwa na Corona  hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kuwa Balozi wa kutangaza Utalii na kutembelea vivutio vilivyopo

 

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.