Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma kuanza kulipa shilingi
261,835,350 wanufaika 8,017 wa mpango wa kunusuru kaya masikni katika dirisha
la Septemba-Oktoba, 2022.
Sekunda Kasese |
Kauli hiyo ilitolewa na Mratibu wa TASAF Halmashauri
ya Jiji la Dodoma, Sekunda Kasese alipokuwa akiongelea utaratibu wa kulipa
wanufaika wa TASAF katika dirisha hili ofisini kwake.
Kasese alisema “katika kipindi cha malipo ya dirisha
la mwezi Septemba hadi Oktoba, 2022 tumepokea shilingi 261,835,350 kwa ajili ya
walengwa 8,017 waliopo katika mitaa 222 ya Jiji la Dodoma. Tuna walengwa 222
wanaolipwa kwa njia ya wakala (OTC) na wakala wa mitandao ya simu. Tuna
walengwa 741 wanaolipwa kwa njia ya mitandao kwa kutumiwa fedha moja kwa moja
kwenye simu. Kuna utaratibu maalum wa kuweza kuwafanya walengwa wanaaopokea
fedha kwa njia ya mitandao na OTC kuna fomu watakazopelekewa ili wasaini
kuthibitisha malipo waliyopokea”.
Katika dirisha hilo, wamepokea kiasi cha shilingi 100,000
sawa na asilimia 1.5 ya mtaa. “Fedha hii inatumika kulipa wenyeviti wa mitaa,
watendaji na wajumbe wa serikali za mitaa na fedha inayobaki inatumika kwa
shughuli za maboresho ya ofisi na shughuli kama kutoa copy na nauli” alisema
Kasese.
Mratibu wa TASAF alisema kuwa katika dirisha hili
wajumbe wa kamati za mpango za jamii (CMC) wamerejeshwa. “CMC wamerejeshwa na kazi
zao ni kushughulikia masuala mbalimbali ya walengwa katika mitaa yao. Na
wataanza kufanya kazi katika dirisha hili kulingana na miongozo ya Mpango wa Kunusuru
Kaya Masikini” alisema Kasese.
Akiongelea maboresho ya warsha za jamii, alisema kuwa
kila dirisha la malipo limekuwa na mada tofauti. “Katika kipindi hiki cha pili
cha awamu ya tatu ya TASAF, wameleta mwongozo ulioboreshwa wa warsha za jamii (community
sessions) malipo ya mwezi Mei-Juni, tulifanya mada ya kwanza ambayo ni
uhawilishaji fedha. Malipo ya Julai-Agosti tulifanya mada ya miradi ya kutoa
ajira za muda na malipo ya mwezi Septemba-Oktoba tutafanya mada ya uwekaji wa
akiba na uchumi wa kaya. Mada hizi zinafundishwa nchi nzima” alisema Kasese.
Aidha, alimshukuru Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji
la Dodoma kwa kuhakikisha fedha hizo zinawafikia walengwa kwa wakati.
MWISHO
Comments
Post a Comment