WAKALA WA MAENDELEO YA UONGOZI WA ELIMU (ADEM) YAJIPANGA KUENDELEA KUTOA MAFUNZO KWA WALIMU WAKUU

 


Na Rhoda Simba Dodoma 

 

WAKALA wa Maendeleo  ya Uongozi  wa Elimu  ADEM  imesema kuwa imejipanga kutoa Mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa Shule kwa Walimu Wakuu wapatao  elfu 17,000, mafunzo hayo yakiwa ni  kutoa mafunzo ya utawala bora kwa wasimamizi wa elimu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

 

Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Mtendaji Mkuu  wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi  wa Elimu  ADEM Dkt Siston Mgullah  wakati akizungumza na  waandishi wa habari jijini Dodoma  kuhusu  utekelezaji  wa majukumu ya wakala huo na vipaumbele vyake kwa mwaka wa  2022/2023.

 

Amesema Katika kipindi cha mwaka 2021/2022, Wakala umeweza kushirikiana na mashirika mengine katika kutoa mafunzo ya Uongozi, Usimamizi na Uthibiti Ubora wa Elimu ikiwemo UNICEF, EQUIP-TZ, World Bank, GPE-LANES, PS3+, Good Neighbors (TZ, Zanzibar Office), Mwanamke Initiatives Foundation (MIF), Aga Khan University (AKU, IED, EA) na Shule Bora.

 

Aidha amesema malengo mengine  ya wakala kwa mwaka 2022/2023 ni pamoja na Kudahili Walimu 2343 katika Kozi za CELMA, DEMA na DSQA, kuandaa Kiongozi cha Mwalimu Mkuu na kuandaa Mwongozo wa Utawala Bora kwa viongozi wa Serikali za Mitaa.

 

 

“Malengo yetu  ni kuimarisha usimamizi wa utoaji wa elimu bora shuleni kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni na miongozo ya elimu, kuziba ombwe la maarifa na ujuzi ambalo kiongozi au mtendaji hakupata katika mafunzo ya awali ya Ualimu na kuongeza idadi ya viongozi wenye maarifa ya uongozi na usimamizi wa elimu,

 

“Katika kipindi cha mwaka 2020/2021, Wakala umefanya tafiti mbalimbali zikiwemo za tathimini ya matokeo ya Mafunzo ya KKK kwa Walimu wa Darasa la III na IV yaliyofanyika Tanzania Bara, utekelezaji wa uthibiti ubora wa shule na utoaji wa mrejesho kwa walimu ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji katika shule za Msingi”amesema Dkt  Mgullah

 

Akizungmzia Kuhusu mafunzo kwa njia ya masafa,amesema kwa sasa wana mradi na  Chuo kikuu  cha Mzumbe kilichopo Morogoro kwa ajili ya kuandaa Moduli za kuendeshea mafunzo ya masafa.

 

 

Akizungumzia kuhusu Ufuatiliaji wa utendaji kazi wa Wakuu wa Shule waliopata mafunzo ya Uongozi na Utawala katika Elimu, ufuatiliaji wa matokeo ya mafunzo ya Stashahada ya uongozi na usimamizi wa Elimu na tathmini ya athari za kozi ya Astashahda ya Uongozi, Usimamizi na Utawala wa elimu iliyofanyika katika mikoa minne.

 

Katika kipindi cha miaka mitano (2018- 2022), Wakala umetoa machapisho ya Moduli ya wajibu na majukumu ya Mjumbe wa Kamati na Bodi ya Shule,Wajibu na majukumu ya Mjumbe wa Bodi ya Chuo cha Ualimu 2022 Moduli ya uthibiti ubora wa Shule wa ndani 2021 na uandaaji na usimamizi wa Utekelezaji wa Mpango wa Jumla wa Maendeleo ya Shule - 2018

 

UTEKELEZAJI WA MALENGO

 

Amesema Wakala umedahili Walimu 1,839 katika mafunzo ya Stashahada ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu (DEMA) na Stashahada ya Uthibiti Ubora wa Shule (DSQA) ili kuwapa ujuzi na maarifa walimu katika usimamizi, ufuatiliaji na tathimini katika elimu.

 

“Wakala umetoa mafunzo ya muda mfupi kuhusu uthibiti ubora wa shule wa ndani, kwa Maafisa 3,860 (REOs, RAOs, DEOs, WEOs) ili kuwajengea uwezo wa kusimamia ufundishaji na ujifunzaji wenye kuleta tija katika elimu,

 

“Wakala umetoa mafunzo ya muda mfupi kuhusu uthibiti ubora wa shule wa ndani kwa walimu 7,612 ili kuwajengea uwezo wa kusimamia ufundishaji na ujifunzaji katika shule wanazosimamia Wakala umeendesha mafunzo ya muda mfupi kwa Walimu Wakuu na Waratibu wa Taaluma 147 kutoka katika Shule za Msingi na Sekondari Zanzibar, chini ya mradi wa Mwanamke Initiative Foundation (MIF).

 

Dkt Magullah amesema Wakala umeendesha mafunzo ya Kamati za Shule kwa Washiriki 126 katika Mkoa wa Songwe ili kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji katika Shule na umeandaa mtaala wa shahada ya menejimenti ya uthibiti ubora wa elimu ili kuimarisha usimamizi na utoaji wa elimu bora katika ngazi zote za elimu.

 

Amesema Wakala umefanya Tafiti sita na kuwasilishwa kwa wadau mbalimbali wa elimu ili kubaini mapungufu na kuandaa mafunzo wezeshi kwa wahusika, wakala umeandaa Moduli 3 katika eneo la Uongozi na Usimamizi wa Shule ili kuendesha mafunzo ya kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa ujenzi wa umahiri kwa walimu wa Shule za Sekondari Zanzibar na umeandika vitabu vya kujenga umahiri katika utekelezaji wa Mtaala wa Sekondari ili kuboresha mbinu za ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya Sayansi, Hisabati na Kiingereza kwa ajili ya Shule za Zanzibar.

 

Nae Mkurugenzi  Mkuu wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu Wa Serikali  Gerson Msigwa amesema Serikali inaweka fedha nyingi kwenye sekta ya elimu nchi nzima ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/23, sekta ya elimu pekee imetengewa Shilingi trilioni 5.8. Chuo hiki ni moja ya juhudi za Serikali za kusimamia ubora wa elimu.

 

“Fedha hizi ni nyingi ambazo zinahitaji usimamizi wa karibu, hivyo wale viongozi wa kwenye taasisi zinazosimamia elimu lazima wawe na ujuzi na mbinu nzuri za kusimamia maendeleo ya elimu ili tuweze kupata thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali,

 

“Viongozi wanaosimamia Taasisi za Elimu wanatakiwa wakasome katika chuo hiki ili wakapate ujuzi wakasimamie vizuri taasisi hizo. Natoa wito kwa waajiri kutosita kuwaruhusu viongozi wa taasisi za elimu kwenda kusoma ADEM”Amesema Msigwa.

 

Mwisho

 

 

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.