ULETAJI WA MAFUTA KWA PAMOJA UNA TIJA-PAC

 


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeeleza kuwa, kazi ya uletaji wa mafuta kwa pamoja nchini inayosimamiwa  na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA)  ina tija kwa Taifa kutokana na sababu mbalimbali ikwemo ya nchi kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta ikiwemo dizeli na petroli.

 

Hayo yamesemwa na Wajumbe wa Kamati hiyo baada ya kukagua miundombinu ya  kushusha na kupima mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam pamoja na hifadhi kubwa ya mafuta ya kampuni ya TIPER ambayo Serikali ni mbia kwa umiliki wa hisa asilimia 50.

 

Ziara hiyo  iliyoongozwa na Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Kheri Mahimbali ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Eng.Felchesmi Mramba, ilifanyika tarehe 14 Novemba, 2022, ambapo Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Japhet Hasunga alisema kuwa, lengo la ziara lilikuwa ni kuona uwezo wa miundombinu hiyo katika kushusha na kuhifadhi mafuta.

 

Mhe. Hasunga alieleza kuwa, baada ya ukaguzi huo Kamati hiyo imejihakikishia kwamba miundombinu iliyopo ya ushushaji na uhifadhi mafuta  ina uwezo wa  kukidhi mahitaj ya nchi hivyo Kamati hiyo imefurahishwa na uwepo wa miundombinu hiyo.

 

Hata hivyo, Kamati hiyo ilitoa wito kwa TIPER kujenga miundombinu ya kuhifadhi mafuta katika maeneo mengine ya nchi  ili kuongeza uwezo wa kampuni na nchi katika kuhifadhi mafuta na pia  kuleta urahisi  katika usafirishaji wa mafuta hayo ndani na nje ya nchi.

 

Awali, kabla ya kufanyika kwa ziara hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PBPA, Erasto Mulokozi, aliieleza Kamati hiyo kuwa, kutoka Wakala huo uanzishwe mwaka 2015 umekuwa na mafanikio mbalimbali ikiwemo kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta yanayotosheleza mahitaji na yenye viwango vya ubora unaohitajika.

 

Manufaa mengine ni Serikali kuweza kupanga ukusanyaji wa mapato kwa kuzingatia takwimu sahihi, kuweza kupanga bei elekezi ya mafuta pamoja na kupata unafuu wa gharama za uletaji wa mafuta nchini kutokana na uagizaji wa mafuta kwa pamoja kwa wastani wa zaidi ya Dola za Marekani milioni 200 Sawa na shilingi bilioni 462 huokolewa kwa mwaka.

 

Aidha alisema kuwa, kutokana na mfumo huo kuleta ufanisi, nchi za jirani pia zinatumia mfumo huo kuagiza mafuta kupitia Tanzania hivyo kuipatia Serikali mapato kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya bandari.

 

Aliongeza kuwa, mfumo huo umesaidia kupunguza upotevu wa mafuta wakati wa kupakua mafuta kutoka melini ambapo wastani wa Tani 1100 ( lita 1,300,000) huokolewa kila mwezi sawa na shilingi bilioni 4.3. 

 

 

 

 

 

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.