SERIKALI KUONGEZA VITENDEA KAZI KWA ASKARI KUKABILIANA NA WANYAMAPORI WAKALI NA WAHARIBIFU

Serikali imesema itaongeza vitendea kazi yakiwemo magari na pikipiki katika Kanda zenye changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu kwa ajili ya kuwezesha kazi ya udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu kunusuru maisha na mali za wananchi wanaoathirika na wanyamapori hao.

 

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja

Hayo yalisemwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja kwa niaba ya Waziri wa Maliasili alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Manyoni Magharibi, Yahaya Massare aliyetaka kujua mikakati ya Serikali ya kudhibiti Tembo wanaovamia vijiji vya Doroto, Kitaraka, Kamenaga, Gurugu, Muhanga na Njirii.

 

Ameongeza kuwa Serikali imekuwa ikitekeleza mkakati wa kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu kwa kuimarisha vituo vya Askari wa Wanyamapori nchini ikiwemo kituo cha askari wanyamapori kilichopo katika kijiji cha Doroto Wilayani Manyoni.

“Wizara imeagiza jumla ya magari 35 na pikipiki 50 ambapo Kanda ya Manyoni itapatiwa gari moja na pikipiki mbili ili kuwezesha udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu” alisema Masanja.

 

Aidha, amefafanua kuwa katika kipindi cha mwaka 2021/22 jumla ya doria 960 zimefanywa na Askari wa Jeshi la Uhifadhi kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo na kuongeza kuwa Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya mbinu rafiki za kudhibiti wanyamapori hao ambapo Askari Wanyamapori wa Vijiji wa wilaya watapatiwa mafunzo maalum katika Chuo cha Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii - Likuyu Sekamaganga Mkoani Ruvuma.

 

Mary Masanja alisisitiza kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kutekeleza mpango wa kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo mengine yenye changamoto nchini kwa kadri fedha zinavyopatikana.

 

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.