SENDIGA: ‘NI AIBU RUKWA KUENDEKEZA IMANI ZA KISHIRIKINA’

Na. OMM Rukwa

Mkuu wa Mkoa, Queen Sendiga akemea kikundi cha matapeli kilichoibuka mkoani humo maarufu kama rambaramba ambao wanasababisha taharuki kwenye jamii wakisaka washirikina.

 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga akihutubia wananchi wa kijiji cha King'ombe wilaya ya Nkasi leo wakati wa mkutano wa hadhara ambapo alikemea kuwepo kwa kikundi cha matapeli maarufu kama rambaramba kinachoendesha msako wa wachawi wilayani humo

Ametoa onyo hilo leo (Alhamisi, Novemba 03,2022) wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji cha King’ombe kata ya Kala wilaya ya Nkasi ambapo kwa siku za hivi karibuni matapeli hao wamekuwa wakichangisha fedha ili waondoshe ushirikina.

 

Sendiga ametoa agizo hilo kufuatia hivi karibuni kutokea kikundi cha watu wanaofanya utapeli kwa kupita kwenye makazi ya watu na kusaka wachawi hatua inayopelekea taharuki kwenye wilaya za Nkasi, Kalambo na Sumbawanga.

 

“Mnaharibu sifa nzuri ya mkoa wetu, watu wanakimbia nyumba zao kwa kuogopa rambaramba kufika kusaka wachawi. Kata hii inaongoza kwa kufanya vikao vya kusaka wachawi. ” alisema  Sendiga.

 

Katika mkutano huo, Sendiga ametoa agizo kwa Jeshi la Polisi kuendesha msako na kuchukua hatua za kuwafikisha mahakamani watu wanaoendeleza vitendo vya kusaka wachawi kwenye makazi ya watu.

 

Naye Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Peter Lijualikali amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa ataongoza kampeni maalum ya kuwasaka watu wanaofanya utapeli kwa kigezo cha kusaka wachawi kwenye makazi ya watu na kukusanya fedha kwa watu.

 

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amefanya ukaguzi wa vituo vya afya Kate na Kala ambavyo vimepokea kila kimoja shilingi Milioni Mia Tano (500,000,000) zilizotokana na tozo ambapo ameagiza Halmashauri kuhakikisha vituo hivyo vinakamilika kabla ya mwaka 2022 kuisha.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga (katikati) akizungumza na viongozi na watumishi wa wilaya ya Nkasi leo alipokagua mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya Kate kinachojengwa kwa fedha za tozo shilingi Milioni 500. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo Peter Lijualikali


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga (katikati) akizungumza na viongozi na watumishi wa wilaya ya Nkasi leo alipokagua mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya Kate kinachojengwa kwa fedha za tozo shilingi Milioni 500. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri William Mwakalambile na kulia Mkuu wa Wilaya hiyo Peter Lijualikali.


Mwisho.

 

 

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.