RC SENDIGA: MIRADI VIPORO YA AFYA KUKAMILIKA KALAMBO

Na. OMM Rukwa

 

Wananchi wa Wilaya ya Kalambo wametakiwa kuendelea kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan ili kuhakikisha miradi ya maendeleo ikiwemo zahanati na vituo vya afya vinakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma.

 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga akishiriki kazi ya ukarabati wa zahanati ya kijiji cha Kapozwa kata ya Mpombwe wilaya ya Kalambo jana alipokwenda kuikagua . Zahanati hiyo iliezuliwa paa lake na upepo mwaka 2020 ambapo Oktoba 20 mwaka huu  wananchi walimwomba Mkuu wa Mkoa asaidie iezekwe upya

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga ametoa wito huo  (Novemba 04,2022) wakati alipofanya ziara ya kufuatilia utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa Oktoba 20 mwaka huu  kwa uongozi wa Wilaya ya Kalambo kuhakisha miradi ya afya ya zamani  inatengewa fedha na kukamilishwa .

“Nimepita kuja kujionea hali ya utekelezaji wa maalekezo yangu ambapo nimeona tayari halmashauri imeanza kutoa fedha na kazi za kukamilisha zahanati ya kijiji cha Kapozwa, kituo cha Afya Kanyezi na Legeza mwendo zimeanza” alisema Sendiga.

Sendiga aliongeza kusema ziara zake kwenye halmashauri zinaendelea ili kuhakikisha Rukwa inaondokana na uwepo wa miradi viporo hususan kwenye sekta ya afya.

“Nawataka watendaji wote wa serikali kwenye mkoa huu  wawajibike ili kuleta matokeo chanya kwa kutatua changamoto za miradi ya maendeleo. Nitahakikisha ninafika maeneo yote kuwatatulia kero wananchi na kuwa hakuna changamoto katika utendaji tutashindwa kuitatua” alisisitiza Sendiga.

 

 

Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Shafii Mpenda (kulia) akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga (kushoto) kuhusu kukamilika kwa ujenzi wa Kituo cha Afya Mwazye kitakachoanza huduma Desemba 2022. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Tano Mwera

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Shafii Mpenda akizungumza na waandishi wa habari katika kijiji cha Kapozwa alisema ataendelea kusimamia shughuli za maendeleo ikiwemo miradi iliyotolewa maelekezo na Mkuu wa Mkoa Sendiga.

Shafii aliongeza kusema nguvu za wananchi zilizotumika kutekeleza miradi ya afya itaenziwa kwa halmashauri kutoa fedha kukamilisha miradi hiyo ambapo ametoa wito kwa awananchi kutochoka kuchangia nguvu zao .

Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa Sendiga amekagua ujenzi wa  kituo cha Afya Mwazye ambacho ameagiza kianze kutoa huduma mwisho wa mwezi huu Novemba huku kituo cha Afya Kanyezi kimepatiwa shilingi Milioni Arobaini  na Kituo cha afya Legeza Mwendo kimepatiwa shilingi Milioni Sitini ili vikalimishwe kabla ya Desemba mwaka huu .

 

Mwisho.


Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.