Na. Haika
Mamuya, WFM, Dodoma
Serikali imejipanga kuhakikisha wananchi wengi
wanapata uelewa wa masuala ya fedha ili kuwawezesha kushiriki katika uchumi
jumuishi na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi.
Kamishna wa
Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja akizungumza na
wanahabari kuhusu maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanayotarajiwa
kufanyika jijini Mwanza yenye lengo la kutoa elimu ya fedha kwa umma, jijini
Dodoma
Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Kamishna wa Idara
ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Charles
Mwamwaja alipokutana na wanahabari kuzungumzia Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa
inatarajiwa kufanyika mkoani Mwanza kuanzia Novemba 21 hadi 26, 2022 yenye
kauli mbiu “Elimu ya Fedha kwa Maendeleo ya Watu”.
Dkt. Mwamwaja alisema Serikali imeweka mikakati
mbalimbali ya kutoa elimu kwa umma kuhusu masula ya fedha ikiwemo maadhimisho
ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa ili kutimiza lengo la Serikali la
kuhakikishasha takriban asilimia 80 ya wananchi wanapata uelewa wa masuala ya
fedha ifikapo mwaka 2025.
“Kutokana na Utafiti wa FinScope wa mwaka 2017
nchini, ni asilimia 48.6 tu ya nguvu kazi ndiyo waliotumia huduma rasmi za
fedha na hivyo kubaki na kundi kubwa la Watanzania ambao hawafaidiki na huduma
hizo na hivyo kukosa fursa za kuboresha maisha yao kupitia shughuli mbalimbali
za kiuchumi na hatimaye kuchangia katika kukuza Pato la Taifa”, alifafanua Dkt.
Mwamwaja.
Alisema Serikali kupitia Wizara ya Fedha na
Mipango imelenga kutumia maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa ili
kujenga uelewa na weledi kwa umma katika matumizi sahihi ya huduma za fedha
zinazotolewa, kujenga uchumi na kuondoa umaskini pamoja na kuongeza upatikanaji
wa huduma za fedha.
Kamishna wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja akimkabidhi kitabu cha elimu ya fedha Mwandishi kutoka kampuni ya TSN, Bi. Nelly Mtema, kulia ni Kamishna Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha, Bi. Dionesia Mjema, jijini Dodoma
Dkt. Mwamwaja alisema wamelenga pia kutoa elimu ya
kuwezesha kumlinda mtumiaji wa huduma za fedha, kuwezesha wananchi kusimamia
vizuri rasilimali fedha na kuwezesha wajasiriamali wadogo kuongeza ujuzi na
matumizi sahihi ya huduma za fedha katika kukuza biashara zao.
“Tunalenga kuimarisha ufanisi wa masoko ya fedha kupitia
elimu ya fedha, kuongeza upatikanaji wa huduma za fedha, kuimarika kwa
utamaduni wa kujiwekea akiba, kukopa na kulipa madeni”, alibainisha Dkt.
Mwamwaja.
Alisema katika kufanikisha hilo Serikali kupitia
Wizara ya Fedha na Mipango itashirikiana na wadau wengine wa masuala ya fedha
zikiwemo wizara, idara, Wakala wa Serikali, wasimamizi wa Sekta ya Fedha,
Taasisi za Fedha, Asasi zisizo za kiserikali, Sekta Binafsi, Bodi za Wataalamu,
Vyama vya Wafanyakazi, Vyombo vya Habari, Taasisi za Elimu na Utafiti,
Washirika wa Maendeleo, Vyama vilele vya Sekta ya Fedha, Makundi ya Watoaji
huduma za fedha na Taasisi za Dini zinazotoa huduma hizo.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi wote hususani wale
wanaoishi Kanda ya Ziwa kushiriki maonesho hayo kikamilifu ili kuweza kupata
elimu hiyo muhimu katika kukuza uchumi wao na wa Taifa kwa ujumla.
Comments
Post a Comment