Na Rhoda Simba, Dodoma
WAKATI suala la ajira
likiwa changamoto kwa baadhi ya wahitimu imeelezwa kuwa kufunguka kwa fursa za
kiuchumi kumewezesha wahitimu wa taasisi ya maendeleo ya jamii Tengeru kupata
ajira katika makampuni ya biashara na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Akizungumza na waandishi wa
habari Jijini Dodoma wakati akiwasilisha utekelezaji na mwelekeo kwa mwaka wa
fedha 2022/2023 Mkuu wa Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru Dkt. Bakari
George amesema upanuzi wa fursa mbalimbali za mikopo ya serikali na kutoka sekta
binafsi kumewezesha baadhi ya wahitimu kujiajiri na kuajiri wengine.
‘’Tunamshukuru Rais, Mhe.
Samia Suluhu Hassan kwa kufungua milango ya ajira ambazo zimewezesha baadhi ya
wahitimu wetu kuajiriwa kama Maafisa Maendeleo ya Jamii, Wahadhiri, Watendaji wa
Kata na Vijiji, Maafisa Mikopo na wengine wameajiriwa kwenye vyombo mbalimbali
ya ulinzi na usalama’’. Amesema
Dkt Bakari amesema kwa
mwaka wa 2022/2023, Taasisi inatarajia kuongeza program 6 za mafunzo
zinazotarajiwa kuanza kutolewa dirisha la Machi 2023 ambapo maandalizi ya
program hizi yamezingatia mahitaji ya soko la ajira kwa sasa na umuhimu wa
kuandaa wahitimu wenye fikra sahihi na uwezo wa kujiajiri.
Ameongeza kuwa Taasisi hiyo
inaendesha program 15 za mafunzo, kwa kipekee, mitaala inayotolewa na Taasisi
imezingatia uwiano kati ya nadharia na vitendo. Hivyo mitaala yote inatekelezwa
kwa kuzingatia dhana tatu ambazo ni uanagenzi, ushirikishwaji jamii na
uanagenzi.
“Ongezeko la udahili
linachagizwa na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika uimarishaji wa
elimu kwa ngazi za msingi na sekondari na umuhimu wa fani ya maendeleo ya jamii
katika muktadha wa upatikanaji wa ajira na mawanda mapana ya kuwezesha
wanafunzi kukabiliana na changamoto za soko la ajira” Amesema.
Kuhusu juhudi za serikali
za kuimarisha mazingira ya ujifunzaji kwa wanafunzi wa kike hapa nchini,
amesema Taasisi ya maendeleo ya jamii Tengeru iliyopo Jijini Arusha kwa mwaka
wa fedha 2022/2023 imeipatia shilingi Bilion 2.3 kwa ajili ya ujenzi wa bweni
la kike ambalo litasaidia kuondoa changamoto wanazokabiliana nazo ikiwemo
vitendo vya ubakaji.
Pia amesema kuwa taasisi
hiyo imeanzisha utaratibu wa kuwachangia fedha wanafunzi wanaoishi mazingira
magumu huku akiwataka watanzania watakaowiwa kutoa michango yao ili wanafunzi hao
waweze kutimiza malengo yao.
“Kwa kipindi cha mwaka wa
fedha 2020/2021, Serikali ya Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan illipatia Taasisi
jumla ya Shillingi 2,700,000,000.00 kwa ajili ya ujenzi wa kumbi pacha za
mihadhara yenye uwezo wa kuchukua idadi ya wanafunzi 1008 ikiwa ni wanafunzi
504 kwa upande mmoja na hosteli ya wasichana ya ghorofa nne yenye uwezo wa
kuchukua wanafunzi wa kike 568“ amesema.
Kwa upande wake Msemaji
mkuu wa Serikali Gerlison Msigwa amesema kuwa serikali kwa kutambua umuhimu wa
elimu tayari imeajiri maafsa maendeleo ya jamii 3000 huku mahitaji yakiwa ni
zaidi ya elfu tano ili jamii iweze kufikiwa na wataalamu Hao.
Taasisi ya Maendeleo ya
Jamii Tengeru inatoa mafunzo ya elimu ya juu na kati na inatekeleza majukumu ya
kuendesha mafunzo ya muda mrefu na mfupi katika nyanja ya Maendeleo ya Jamii,
Upangaji na Usimamizi wa Miradi na Jinsia na Maendeleo pamoja na kufanya tafiti
na kutoa ushauri elekezi katika masuala ya maendeleo ya jamii na ustawi wa watu
kwa ujumla
Mwisho
Comments
Post a Comment