Na: Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
09/11/2022
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imesaini mkataba na chuo Kikuu cha
Jagiellonian kilichopo nchini Poland kwa ajili ya kushirikiana katika kubadilishana
ujuzi wa kutoa huduma za kibingwa za matibabu na upasuaji wa moyo.
Mkataba
huo ambao utaanza kutumika mapema mwakani ulisainiwa jana jijini Dar es Salaam
na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter
Kisenge na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Jagiellonian cha nchini Poland Prof.
Bartlomiej Guzik.
Akizungumza
na waandishi wa habari hizi Dkt. Kisenge alisema JKCI imesaini mkataba na chuo
hicho ili kuweka ushirikiano ambao umelenga kuongeza wigo katika kutoa tiba ya magonjwa
ya moyo pamoja na upasuaji wa moyo katika Taasisi hiyo.
“Tumesaini
makubaliano ambayo yatawawezesha wataalam wetu kwenda nchini Poland kwa ajili
ya kujifunza namna wenzetu wanavyotoa huduma za matibabu ya moyo lakini wao pia
watakuja hapa kwetu kuona na kujifunza jinsi tunavyotoa huduma za tiba na
upasuaji wa moyo”,
“katika
ushirikiano huu pia tumekubaliana wenzetu hawa watatuletea wataalam ambao
watashirikiana nasi katika kuwahudumia wagonjwa kwa kufanya matibabu ya
kibingwa ya upasuaji wa moyo hasa kuzibua mishipa ya damu ambayo imeziba,
kubadilisha valvu za moyo bila kupasua kifua upasuaji unaoitwa TAVI procedure ambao kwa hapa nchini
kwetu bado haujaanza kufanyika”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt.
Kisenge alisema JKCI imeongeza wigo wa kuwa na ushirikiano na mashirika
yanayotoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kutoka nchi 18 ikiwemo nchi
hiyo ya Poland ambayo itaanza rasmi kubadilishana ujuzi na wataalam wa Taasisi
hiyo mapema mwakani.
“Tutaendelea
kuongeza ushirikiano huu wa kubadilishana uzoefu na nchi nyingine ambazo
tunaamini zinatoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo nia ikiwa ni kuifanya
JKCI kutoa matibabu ya kibingwa ya magonjwa ya moyo katika Afrika yote”,
alisema Dkt. Kisenge
Naye
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Jagiellonian kilichopo nchini, Poland Prof. Bartlomiej
Guzik alisema wamevutiwa kufanya kazi na wataalam wa afya wa JKCI ili kwa
pamoja waweze kutoa huduma za kibingwa za matibabu na upasuaji wa moyo kwa
wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.
“Kujenga
uhusiano baina yetu na JKCI kutasaidia kuboresha huduma za kibingwa za matibabu
na upasuaji wa moyo lakini pia kutaongeza ubobezi kwa wataalam hawa wa afya”,
alisema Prof. Bartlomiej.
Comments
Post a Comment