ASKOFU MKUU AICT TANZANIA AWEKWA WAKFU

Askofu Mkuu wa Kanisa la AICT Tanzania Musa Masanja Magwesela amesimikwa 6 Novemba, 2022 baada ya kuchaguliwa katika mkutano wa Sinodi kuu ya Kitaifa iliyofanyika mwezi wa tisa mwishoni katika kanisa la AICT Buzuruga Mwanza.

 


Katika tukio hilo la kuwekwa Wakfu ambalo lilihudhuriwa na Viongozi mbalimbali kutoka Serikalini na watumishi wa Mungu, pia alisimikwa Askofu Mkuu Msaidizi ambaye ni Askofu wa Dayosisi ya Shinyanga Zakayo Bugota.

 

Tukio la kuwekwa Wakfu kwa Askofu Mkuu na Msaidizi wake lilifanyika katika kanisa la AICT Makongoro kuanza asubuhi saa 2 hadi saa 8 mchana, lilihudhuriwa na umati mkubwa wa waumini kutoka madhehebu mbalimbali Mkoani Mwanza na nje.

 

Akizungumza kwa niaba ya Serikali Mgeni Rasmi wa sherehe hizo Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko alimpongeza Askofu Mwageswela na Msaidizi wake Askofu Bugota kwa kuaminiwa katika nafasi hizo na kuomba wawaunganishe waumini wa Kanisani hilo ili liendelee kuongezeka kwa idadi ya watu.

 

"Baba Askofu Mkuu na Msaidizi wake mmeaminiwa sana, mmepewa nafasi ya kumtumikia Mungu na kanisa la AICT Tanzania, fanyeni kazi ya kuhubiri Neno la Mungu kiroho na kimwili ili kanisa hili liwe na maendeleo makubwa" alisema Waziri Dkt. Biteko.

 

"Serikali ya Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan iko bega kwa bega na wewe katika kuwasaidia wananchi wapate kuponywa katika mambo ya kiroho na kimwili maana kanisa lina nafasi kubwa katika maisha ya mtu" 

 

Dkt. Biteko alisema anaamini katika uongozi wa Askofu Mkuu Musa Magwesela na Msaidizi wake Askofu Zakayo Bugota, ndio maana wamepewa miaka mingine kuongoza kanisa hilo katika muhula wa pili.

 

Akitoa salama za kanisa baada ya kuwekwa Wakfu Askofu Mkuu Magwesela alisema wanashukuru sana kupewa nafasi hiyo kumtumikia Mungu na kuomba kupewa ushirikiano ili waweze kutimiza matarajio ya kanisa. Huku akiomba Serikali kutatua migogoro iliyopo kwenye umiliki wa viwanja mali ya kanisa ila kuna watu wanaviingilia kinyemela.

 





MWISHO

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.