Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera ,Bunge na Uratibu George Simbachawene amesema Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na Marais wastaafu watatunukiwa tuzo maalum kwa kufanikisha Sensa katika vipindi vya uongozi.
Amezungumza hayo leo Jijini, Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuelekea kwenye Uzinduzi wa Matokeo ya Mwanzo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 utakao fanyika katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Oktoba 31 Oktoba, 2022 .
"Katika uzinduzi huu Mgeni Rasmi atakuwa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan. Sensa ya Watu na Makazi hufanyika mara moja kila baada ya miaka kumi na matokeo yake ndio yanayotumika katika kufanya maamuzi yote muhimu yanayohusu maendeleo ya nchi kwa kipindi cha miaka kumi hadi Sensa nyingine." amesema Simbachawene
![]() |
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma kuelekea kwenye uzinduzi wa Matokeo ya Mwanzo ya Sensa ya Watu na Makazi 2022. |
Aidha, amesema Rais Samia pia atazindua Mwongozo Maalum wa Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 lengo lake kuu ni kuhakikisha matokeo ya Sensa yanatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
"Matokeo haya ni muhimu sana kwa makundi yote katika jamii, wafanyabiashara, wakulima, wafugaji na hasa kwa Serikali yetu inayoongozwa na Rais Samia kwani Serikali itaweza kupanga mipango yake kwa ajili ya maendeleo ya wananchi kulingana na idadi, mahitaji na mazingira wanamoishi." ameongeza Simbachawene
Viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo mawaziri na manaibu waziri, Makatibu wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu wa Serikali zetu zote mbili, Wabunge , Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Zanzibar, viongozi wa vyama vya Siasa na wawakilishi wa makundi mbalimbali katika jamii watashiriki katika tukio hilo.
Mwisho.
Comments
Post a Comment