MAENEO YALIYOMEGWA KWENYE HIFADHI YAPANGIWE MPANGO WA MATUMIZI YA ARDHI

 


Na Munir Shemweta, WANMM NJOMBE

 

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ametaka maeneo ya yanayomegwa kwa ajili ya kupatiwa wananchi waliovamia hifadhi yapangiwe mpango wa matumizi ya ardhi na kutolewa hati kwa wamiliki wake.

 

Dkt mabula alitoa kauli hiyo oktoba 27, 2022 katika kijiji cha Mpanga kilichopo wilaya ya Wanging'ombe wakati timu ya mawaziri nane wa wizara za kisekta inayoshughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 ilipotembelea mkoa wa Njombe ikiwa ni  mfululizo wa ziara zake kawenye mikoa ya Tanzania Bara.

 

Kijiji cha Mpanga ni moja ya vijiji 11 vilivyopo wilaya ya Wanging'ombe na Makete mkoani Njombe ambavyo vimemegewa eneo kutoka hifadhi ya Pori la Akiba la Mpanga Kipengele.

 

Dkt Mabula alisema, serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeridhia baadhi ya vijiji kwenye mkoa wa Njombe kubaki maeneo ya hifadhi za Mapori ya Akiba ingawa wananchi wake waliingia bila ridhaa ya serikali.

 

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, ili kuondokana  na migogoro ya ardhi  vijiji vilivyomegewa maeneo vitapimwa na kumilikishwa ili wamiliki kujua mipaka sambamba na kuweza kutumia hati kukopa fedha benki na fedha kutumika kuboresha shamba au mifugo.

 

"Kinachofanyika hapa siyo tu kutoa maeneo, eneo linatolewa lakini liwekewe mpango mzuri na endelevu ili kuona jinsi gani mnaweza kutumia ardhi mliyopewa kwa faida na kwa sababu tunaongezeka basi mpango uwe mzuri na endelevu" alisema Dkt Mabula.

 

Amebainisha kuwa, ni lazima maeneo yanayopangwa yaanishwe matumizi yake kama vile maeneo ya akiba, hifadhi, makazi na uwekezaji na kutaka wakati wa utekelezaji wataalamu wazingatie mpango wa matumizi katika maeneo hayo.

 

Timu ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta ambayo inashughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi kwenye vijiji 975 imemaliza ziara yake katika mkoa wa Njombe ukiwa ni mkoa wa 22 kati ya 26 ya Tanzania Bara na inaendelea na ziara yake katika mkoa wa Ruvuma.

MWISHO

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.