Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WAKAZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa
kujali afya ya mifugo (Mbwa na Paka) kwa kuhakikisha wanapata chanjo na
matibabu ili kuepuka vifo na madhara yatokanayo na kichaa cha Mbwa.
![]() |
Mkuu wa Divisheni ya Kilimo mjini katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Yustina Munishi |
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Divisheni ya Kilimo
mjini katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Yustina Munishi alipokuwa akitoa
ushauri kwa wakazi wa jiji hili katika maadhimisho ya siku ya kuzuia ugonjwa wa
kichaa cha Mbwa duniani.
Munishi alisema kuwa jamii inatakiwa kuchukua
tahadhari zote dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha Mbwa. “Ni muhimu kuhakikisha afya
ya mifugo hasa Mbwa na Paka inazingatiwa katika maeneo yetu kwa sababu ugonjwa
wa kichaa cha Mbwa unasababisha madhara na vifo kwa binadamu na Mbwa wenyewe.
Mfano uwepo wa Mbwa katika makazi yetu ni faida kwa sababu anatusaidia ulinzi
lakini pia ni mnyama rafiki katika jamii kama alivyo Paka. Hivyo, jamii ina
wajibu wa kuwatunza kwa kuhakikisha wanapata chanjo zote na matibabu ili wawe
na afya njema na tuendelee kunufaika nao” alisema Munishi.
Aidha, aliipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa
maadhimisho ya siku ya kuzuia kichaa cha Mbwa duniani.
Siku ya kuzuia kichaa cha Mbwa duniani
huadhimishwa kila mwaka tarehe 28 Septemba, kwa
lengo la kuhamasisha jamii kutokomeza ugonjwa wa kichaa cha Mbwa kwa kufanya kampeni za chanjo na kutoa elimu kwa umma juu
ya ugonjwa huu hatari.
Mwaka huu maadhimisho hayo yameongozwa na kaulimbiu isemayo Afya moja: Bila vifo.
MWISHO
Comments
Post a Comment