Na Fred Kibano, Dodoma
Serikali imewaagiza wakuu wa mikoa kote nchini kusimamia kwa
ukamilifu zoezi la kuwasajili wakulima kwa ajili ya zoezi la mfumo wa utoaji wa mbolea ya ruzuku
kwa msimu wa mwaka 2022/20223.
![]() |
Waziri Innocent Bashungwa |
Hayo yalisemwa na Innocent Bashungwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
TAMISEMI wakati akitoa salamu kwenye kikao maalum kati ya Ofisi ya Rais
TAMISEMI na Wizara ya Kilimo kilichowahusisha wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa katika ukumbi wa St. Gaspar jijini Dodoma jana.
“Lipo suala la wakulima, waheshimiwa wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa, ili tuweze kupeleka huduma kwa
mkulima, kuna suala la kusajili wakulima wetu, Wizara ya Kilimo inatutegemea
sisi ili kuhakikisha suala la kuwasajili wakulima linafanikiwa kwa kiasi
kikubwa” alisema Bashungwa.
Bashungwa amesema pia lengo la kikao hicho ni sehemu ya
kujipanga katika kuhakikisha utekelezaji wa dira na maelekezo ya Mhe. Rais
Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha yanatokea mapinduzi chanya kwa wakulima
kote nchini.
Akitoa hotuba katika kikao hicho, Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe amesema wizara
yake inazingatia teuzi za Bodi za Kilimo kuwa na mkuu wa mkoa kama mjumbe kwasababu wao pamoja na wakuu wa wilaya, makatibu tawala wa mikoa ndio kama mikono ya Wizara ya Kilimo na lazima wahusishwe kwenye
masuala yote ya kilimo kwenye maeneo yao.
Bashe amesema katika mwaka huu wa fedha Wizara ya Kilimo
itaajiri Wahandisi wa umwagiliaji ambao watapelekwa katika kila halmashauri
zoezi ambalo litakwenda sambamba na kuwapatia magari kwa ajili ya ufuatiliaji
wa kazi zao.
Pia wizara hiyo inaendelea kugawa pikipiki kwa Maafisa
Ugani ambazo idadi yake itafikia 7,000 kwa ajili ya maafisa hao ngazi ya halmashauri
Tanzania Bara kuweza kuwahudumia wakulima kwa kuongeza uzalishaji na kupunguza
gharama za kilimo.
Aidha, amesema mfumo mpya wa ruzuku ya utoaji wa
mbolea unatumia kanzi-data kuanzia ngazi ya kitongoji, kijiji hadi ngazi ya juu
na mpaka sasa jumla ya wakulima halali 1,297,240 wamekwishasajiliwa.
Katika hatua nyingine Waziri Bashe amesema wizara yake inatarajia kujenga maghala
62 mapya kwa ajili ya kuhidhia mazao ambapo mkoa wa Ruvuma utakuwa na maghala
31sawa na asilimia 80 ya maghala yote.
Kwa upande wake Mkurugeni wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea
nchini (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo amesema jumla ya shilingi Bilioni 150
zimetolewa na Serikali katika mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kutekeleza Mpango
wa utoaji wa mbolea ya ruzuku kwa wakulima nchini ili kuongeza uzalishaji wa
mazao, kupunguza gharama ya mbolea, kulinda usalama wa chakula, kuongeza
upatikanaji wa bidhaa za viwanda, kuongeza fedha za kigeni na kuimarisha
upatikanaji wa ajira nchini.
Akiongea kwa niaba ya wakuu wa mikoa mwenyekiti wa wakuu wa mikoa ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa
Arusha, Mhe. John Mongela amesema kuwa suala la wakulima ni sehemu ya
jukumu lao na hivyo watalitekeleza kama ilivyoagizwa.
“Sisi kama unavyotuona hii ni sehemu ya
wajibu wetu, kwa niaba ya wenzangu nikuhakikishie hatuwezi kurudi nyuma
tunaunga mkono hii kazi na tunaenda kuitekeleza kama inavyotakiwa” alisema Mhe.
Mongela.
Kikao kazi hicho cha siku moja kilikuwa na lengo la
kuwakutanisha Viongozi hao na wizara mbili ili kuona namna ya kumsaidia mkulima
nchini na kukuza ustawi wa uchumi wa mazao kwa ujumla.
Chanzo: www.tamisemi.go.tz
Comments
Post a Comment