Na Rhoda Simba, Dodoma
SAKATA la ndugu wa marehemu Richard Bukombe mkazi wa Miyuji jijini
Dodoma aliyefariki dunia kwa kile kinachodaiwa kugongwa na gari mali ya jeshi
la Magereza limechukua sura mpya baada ya wanafamilia kumtaka Mkuu wa Jeshi la
Magereza, kutowakingia kifua waliohusika.
Aidha, wameiomba Tume ya Haki za Binadamu pamoja na Kituo cha Haki za
Binadamu na Msaada wa Kisheria (LHRC) kuingilia kati sakata hilo ili kifo cha
ndugu yao kipatiwe haki.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa kwa niaba ya familia
mdogo wa marehemu Bukombe Bulole, alisema pamoja na kuzika mwili wa ndugu yao
bado hawata kata tamaa ya kupata haki ya ndugu yao.
Amesema baada ya kuuzika mwili wa marehemu walifuatilia katika hospitali
ya rufaani ya mkoa wa Dodoma ambapo ilibainika kuwa mwili wa ndugu yao uliletwa
na kutelekezwa katika chumba cha kuhifadhia maiti na askari wa Jeshi la
Magereza.
“Kamishna anapaswa kulifanyia kazi hili kwani lipo mikononi mwake
asiwape kazi viongozi wake wa juu kwa ajili ya kuwalinda wahahusika, tunamuomba
sana atusaidie hakuna haja sisi kumfuata waziri mkuu au Rais Samia Suluhu
Hassan afanye kitu ambacho ni jukumu la mteule wake”amesema Bukombe
Amesema kuendelea kukaa kimya kwa jeshi la Magereza kunazidi kuwapa hofu
kuwa ndugu yao alipogongwa na gari hakuwa amekufa bali wao ndiyo waliomalizia
ili kuondoa ushahidi.
“Ndugu wanahabari sheria ya usalama barabarani kifungu cha 57 ii b
kinamtaka mtu yeyote atakaye sababisha ajali aripoti kituo cha polisi ndani ya
saa 12 ila sheria itamsamehe akichelewa endapo kutokana na ajali hiyo atakuwa
hawezi kutimiza takwa la sheria hiyo.
“Lakini pia kifungu cha 40 sura ya168 iliyofanyiwa marekebisho mwaka
2002 inasema kwamba mtu yeyote atakayesababisha majeruhi au kifo kwa mujibu wa
sheria ya usalama barabarani atakuwa ametenda kosa la jinai”amesema
Amesema kwakuwa askari Magereza ni miongoni mwa vyombo vinavyohakikisha
sheria ya nchi haivunjwi na kwa kutoripoti ajali ile kituo cha polisi wamevunja
sheria.
“Hivyo askari Magereza ambao ni wasimamizi wa sheria za nchi wametenda
kosa la jinai na tunawaomba viongozi wao wawafikishe mahakamani mara moja bila
kusumbua vyombo vingine vya usalama kuchunguza jambo hilo”amesisitiza Bukombe
Vilevile, alisema familia inamuomba Kamishna wa Magereza aige mfano wa
Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge na Uratibu George Simbachawene
alivyoruhusu sheria ifuate mkondo wake kwa mtoto wake ambaye alivunja sheria za
nchi.
Bukombe, alisema toka ajali imetokea Septemba 13, mwaka huu hadi leo hii
ni zaidi ya siku 14, zimepita bila kuona chochote kilichofanywa na Magereza
zaidi ya danadana za kivuta muda ili wasahau na kuacha kufuatilia jambo
hilo.
Marehemu Richard Bukombe, maarufu kwa jina la Baba Paroko anadaiwa
kugongwa na gari mali ya Jeshi la Magereza (Land cruzer pick up) Septemba 13,
mwaka huu jirani na eneo la Twiga hotel Msalato jijini hapa.
Kwa mujibu wa ndugu zake wanadai aligongwa na gari hilo mali ya Magereza
majira ya saa 12:30 jioni ambapo baadhi ya askari wa jeshi hilo walimchukua na
kuondoka naye na baadaye mwili wake kukutwa umetelekezwa mochwari.
Mkuu wa Jeshi la Magereza mkoa wa Dodoma Kenneth Mwambije, alipoulizwa
kuhusu tukio hilo alikiri kuwa analifahamu kama ambavyo watu wengine
wanavyolisikia lakini akasisitiza kuwa watu wa kulitolea ufafanuzi ni makao
makuu ya Jeshi hilo.
Wiki iliyopita Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Yussuf Hamad Masauni,
alipoulizwa kuhusu tukio hilo alisema anaomba kwanza kukutana na wanafamilia
hao ili kusikiliza malalamiko yao.
Mwisho
Comments
Post a Comment