RAIS SAMIA AZINDUA CHAMA CHA MAWAKILI WA SERIKALI,AWATAKA KUTOA ELIMU KWA UMMA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amemuagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia upya Sheria za uwekezaji pamoja na biashara nchini ili kukabiliana na migogoro inayotokana na Sheria hizo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akibonyeza Kitufe kwenye laptop kuzindua mfumo rasmi wa Kieletroniki wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (OAGMIS), nembo ya Ofisi hiyo pamoja na Chama cha Mawakili wa Serikali katika Mkutano Mkuu wa Mawakili wa Serikali



Rais Samia ametoa agizo hilo leo wakati akizindua Chama cha Mawakili wa Serikali katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete.

Aidha, Rais Samia amesema ni vyema Mawakili wa Serikali wawe makini na kuharakisha kusikiliza migogoro inayokinzana na Sheria za uwekezaji ili kupunguza kupelekana Mahakamani na wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa nchini.

Rais Samia amesema kufanya hivyo kutasaidia kupunguza kesi za uwekezaji, kulinda uwekezaji nchini na kupanua wigo wa kukuza uwekezaji, kukusanya mapato na hivyo kukuza uchumi kwa maslahi ya taifa.

Kwa upande mwingine, Rais Samia amewataka Mawakili wa Serikali kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu bila kukiuka haki za wananchi na kuwasaidia kutatua kero zao ambazo hazihitaji kufikishwa mahakamani.

Rais Samia pia ametoa wito kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu pamoja na Mawakili wote wa Serikali kuendelea kutoa elimu kwa umma hususan sheria zinazowagusa wananchi na kuwaelekeza taratibu za namna ya kupata haki zao.

Vile vile, Rais Samia amesema utoaji wa elimu utapunguza mrundikano wa mashauri ambayo hayana ulazima wa kufikishwa mahakamani kwa ajili ya utatuzi na hivyo pia kuchangia kupunguza mrundikano wa mahabusu.

Rais Samia amewataka Wakuu wa Mikoa kutumia Kamati za Ushauri wa Kisheria zilizoanzishwa katika ngazi zote za Mikoa na Wilaya nchini kupunguza malalamiko ya wananchi na mashauri dhidi ya Serikali.

Zuhura Yunus
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Viongozi mbalimbali pamoja na Mawakili wa Serikali kabla ya kuzindua Chama cha Mawakili wa Serikali, nembo na Mfumo rasmi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali





Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.