Na. Dennis Gondwe, DODOMA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan
amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI kuwachukulia hatua wale wote
waliotumia vibaya fedha za lishe na kukwamisha malengo ya serikali katika kukabiliana
na changamoto za lishe nchini.
Agizo hilo alilitoa alipokuwa akihutubia halfa ya
utiaji saini mkataba wa usimamiaji wa shughuli za lishe tukio lililofanyika
katika ukumbi wa kisasa wa mikutano wa jengo la kitega uchumi la Halmashauri ya
Jiji la Dodoma lililopo Mji wa serikali Mtumba jijini hapa.
Rais Samia alisema “nakuagiza Waziri wa TAMISEMI, wote
waliotumia vibaya fedha za lishe au kuzitumia kwa malengo tofauti wachukuliwe
hatua na ripoti yake niipate”.
Akiongelea lengo la halfa hiyo, alisema kuwa ni
kutatua matatizo ya lishe nchini. “Ndugu zangu, lengo ni kutatua matatizo ya
lishe yaliyopo katika maeneo yenu na hasa wanajamii, kuelimisha na kuhamasisha
umma kuhusu masuala ya lishe na lishe bora kwa kutumia jumbe mbalimbali na
kutoa ushauri kwa wananchi na hasa makundi yanayolengwa” alisema Rais
Samia.
Kuhusu umuhimu wa lishe bora, alisema kuwa ni muhimu
kwa jamii hasa wajawazito, watoto na wanawake walio katika umri wa uzazi,
wazee, na vijana katika rika ya balehe. “Sasa ukitizama tunaanza na wajawazito
kuwapa lishe bora ili watoe watoto wenye afya. Lakini mtoto mwenye afya akisha
kuzaliwa tunahitaji kumtunza mtoto huyo nae akifika umri, akiitwa balehe
anahitaji kutunzwa pia. Anahitaji kutunzwa ili kama ni mwanamke au mwanaume
waje wazae pia watoto wenye afya. Sasa tuangalie ulimwengu wetu sasa hivi. Mama
mjamzito tunahangaika nae, watoto wakishazaliwa hawawezi kujisaidia, inaeleweka
lazima tuwatunze, watoto balehe. Hebu tufanye utafiti tunakosea wapi? Kwa nini
wanakuwa na lishe mbovu?
Kwa nini kunakuwa na changamoto ya lishe, je ni
mitindo ya maisha nataka niwe ‘sixpacks’, nataka sijui niwe ‘slim’, nisizidi
kilo ngapi…wakifika wakati wa kuwajibika kuja kuzaa kuongeza ‘society’
wanahangaika. Mara supu ya pweza…Tunatatizo na mnalijua mnalificha. Watafiti
fanyeni utafiti. Tunatatizo na tatizo hili kwa sababu halisemwi ni siri
linaumiza zaidi vijana wetu, mara ndo udongo wa kongo…tatizo kubwa liko kwenye
lishe” alisisitiza Rais Samia.
Akiongelea ukubwa wa tatizo la lishe, Rais Samia
alisema kuwa matokeo yake ni kuwa na taifa goigoi. “Nasema haya kwa sababu
nilishasema kwamba tukiacha hali hii tunaenda kuwa na taifa goigoi. Tunaenda
kuwa na taifa lenye watu na si rasilimali watu, ni watu ambao ni mzigo kwa
taifa siyo watu ambao watazalisha kwa ajili ya taifa. Kuzalisha mali, kusimamia
uchumi, lakini pia kuzalisha watu ili taifa hili liendelee, tutafika pahali
hapa hatumjui mke nani mume nani” alisema Rais Samia kwa masikitiko.
Akimkaribisha Rais Samia kuhutubia, waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais TAMISEMI, Innocent Bashungwa alianza kwa kuipongeza Halmashauri
ya Jiji la Dodoma kwa ujenzi wa ukumbi bora na wa kisasa kwa hadhi ya makao
makuu. “Ukumbi huu ni bora na unapendeza na tupo hapa ‘very confortable’.
Tuwapongeze sana wenzetu upande wa Jiji la Dodoma” alisema Bashungwa.
Akiongelea shughuli ya tathmini ya 6 ya utekelezaji wa
mkataba wa lishe alisema kuwa mkataba huo ni utekelezaji wa agizo la Rais.
“Utekelezaji huu uliuasisi mwenyewe mwaka 2017/2018 na ulielekeza usimamizi na
utekelezaji wa shughuli za mkataba wa lishe ufanywe na waheshimiwa wakuu wa
mikoa” alisema Bashungwa.
MWISHO
Comments
Post a Comment