SERIKALI KUSHIRIKIANA NA WADAU KUKABILI MAAFA.

 Na Mwandishi wetu- Dodoma

Serikali imesema itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika mapambano dhidi ya maafa ambayo hujitokeza katika maeneo mbalimbali nchini na kusababisha athari.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja Jenerali Michael Mmanga, Jijini Dodoma wakati akifungua  Warsha ya Kuandaa Taarifa ya Nchi ya Utekelezaji wa Mkakati wa Kimataifa wa Sendai (2015-2030).

Mkurugenzi huyo alisema uwepo  wa mkakati wa Nchi wa upunguzaji wa athari za maafa (2020-2025) na uwezo wa jamii katika kupunguza, kujiandaa na kukabili maafa umeongezeka.

 “Nchi yetu imekuwa ikishuhudia kuongezeka kwa matukio ya majanga ambayo yamekuwa yakisababishwa na sababu mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi na shughuli za kibinadamu,”alisema Meja Jenerali Mmanga.

Pia aliongeza kwamba  pindi maafa  yanapotokea husabibisha madhara mbalimbali ikiwemo vifo, majeruhi, upotevu na uharibifu wa mali na miundombinu ya umma iliyotumia gharama kubwa kujengwa.

“Kwa ujumla, majanga haya yamekuwa yakisababisha matokeo hasi katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi kutokana na kupotea kwa mafanikio yaliyopatikana kwa muda mrefu na hivyo, kuzorotesha hatua za maendeleo,”aliongeza.

Aidha kufuatia zoezi la sensa ya watu na makazi inayoendelea nchini Meja Jenerali Mmanga aliwahimiza washiriki wa warsha hiyo kujitokeza kuhesabiwa ili kuiwezesha Serikali kupanga miradi ya maendeleo kwa manufaa ya Taifa.

“Zoezi la sensa linaendelea kwa wale ambao bado hawajahesabiwa hivyo naendelea kuwahamasisha kupata idadi halisi ya watu waliopo nchini itakayowezesha kuandaa rasilimali na mipango halisi inayokidhi mahitaji ya watu nchini,”alihimiza Mkurugenzi huyo.

Naye Mshauri Mkuu Afrika kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupunguza Hatari za Maafa (UNDRR) Bwa. Hachim Badji aliipongeza serikali kwa kuendelea kuchukua hatua za kukabili maafa pamoja na kushirikisha taasisi mbalimbali.

“Warsha hii itumike kama fursa ya kubadilishana taarifa,uzoefu, mafanikio ambayo tueyapata tagu mwaka 2015 tuweze kujua wapi tulipotoka, tulipo na tunapoelekea katika mapambano haya  kama UNDRR tutatoa ushirikiano kufikia malengo yaliyowekwa,” alisema Bwa. Badji.

Kwa upande wake Afisa Mwandamizi Uratibu wa Maafa kutoka Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Bwa. Juvenal Kisanga alibainisha kuwa WFP imekuwa ikifanya kazi kwa kushirikiana na serikali kuhakikisha maafa yanadhibitiwa na wananchi kufanya shughuli zao katika mazingira salama kwa mujibu wa mpango wa maendeleo endelevu ifikapo 2030.

“UN kupitia wanachama wake waliopo hapa nchini tunafanya kazi kwa kMufuata vipaumbele vya Serikali kwa sababu yenyewe inatengeneza sera, mikakati na mipango ya kupunguza athari za maafa na sisi tunaunga mkono ili kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao,”alieleza Afisa huyo.

###MWISHO###

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.