Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Laban Thomas amesema takwimu ya kitaifa ya sensa inaonesha kuwa hadi kufikia Agosti 26 mwaka huu saa moja asubuhi Mkoa wa Ruvuma ulikuwa umefikia asilimia 63 ya lengo la Kuhesabu zaidi ya kaya 450,000.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas alipowasili katika ofisi za Mtendaji Kata ya Peramiho Halmashauri ya Songea kwa ajili ya ukaguzi wa zoezi la sensa katika baadhi ya mitaa ya Kata hiyo |
Kanali Thomas amesema hayo wakati anazungumza na wananchi wa
Peramiho nje kidogo ya Mji wa Songea alipofanya ziara ya kukagua zoezi la sensa
linaloendelea nchini kote.
Amesema kutokana na takwimu hizo za kitaifa Mkoa unakwenda vizuri
ambapo ametoa rai kwa wananchi kuendelea kushirikiana na makarani kwa
kujitokeza kuhesabiwa ili Mkoa uweze kupata takwimu za sensa za watu za kutosha
ambazo zitaisaidia serikali kupanga mipango ya maendeleo.
Hata hivyo Kanali Thomas amesema anatamani Mkoa wa Ruvuma uvunje
rekodi za kitaifa kwenye majumuisho ya sensa kwa kuongoza kitaifa.
RC Thomas amewapongeza watendaji kwa usimamizi mzuri katika zoezi la sensa ambapo amewataka viongozi wa Halmashauri zote kuendelea
kuwaelimisha wananchi wajitokeze
kuhesabiwa ili kufikia malengo ya Mkoa na taifa kwa ujumla
“Matumaini yangu tuakwenda vizuri
niwaombe wananchi wenzangu endeleeni kujitokeza ili tupate data sahihi,
data hizi zina manufaa kwetu na kwa
taifa letu”alisema RC Thomas.
Naye Mkurugenzi wa Halmashaur ya Wilaya ya Songea Neema
Maghembe ameeleza Halmashauri hiyo yenye Kata 16, inatarajia kuhesabu
kaya zaidi ya 36,000, na kwamba
hadi kufikia Agosti, 25, wameweza kuhesabu kaya zaidi ya 28,000.
“Nikuhakikishie Mkuu wa Mkoa zoezi hili linakwenda vizuri na watu
wanajitokeza kuhesabiwa, hata kaya uliotembelea umekuta zoezi linakwenda
vizuri” alisema Bi maghembe.
Mkoa wa Mkoa wa Ruvuma, anaendelea na ziara ya kukagua
maendeleo ya zoezi la sensa ya watu na makazi katika Halmashauri za Mkoa
wa Ruvuma.Zoezi hili lilianza Agosti, 23, 2022 na linatarajiwa
kukamilika Agosti, 28 mwaka huu.
Imeandikwa na Albano Midelo
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma
Agosti 26,2022
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Thomas Laban akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Peramiho ambao tayari walikuwa wamehesabiwa katika zoezi la sensa ambalo linaendelea nchini kote |
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Thomas Laban akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Peramiho ambao tayari walikuwa wamehesabiwa katika zoezi la sensa ambalo linaendelea nchini kote |
Comments
Post a Comment