Na Rhoda Simba Dodoma,
WAZIRI wa Maliasili na Utalii Dkt. Pindi Chana amewaasa Makamanda,Maafisa na Askari wa Uhifadhi (TFS) kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutatua kero za
uhifadhi na migogoro baina ya wananchi .
Akizungumza leo jijini Dodoma katika mafunzo ya makamishina, makamanda na askari wa uhifadhi wa misitu ya kila mwanzo wa mwaka wa fedha, ambapo amewataka kusimamia sheria pamoja na kutowaruhusu wavamizi wasipewe nafasi kuingia katika hifadhi za misitu kwa maendeleo ya Taifa na watu wake.
"Nawaelekeza kusimamia sheria na shirikianeni na kamati
za ulinzi na usalama za Mikoa na Wilaya kuhakikisha wavamizi wote wanaondoka na
kuacha hifadhi za misitu zikiwa salama, ndugu zangu jambo hili la uvamizi
katika maeneo ya misitu tusiliruhusu na hili ni eneo ambalo tutawapima"
Amesema Dkt Pindi Chana.
Aidha,Dkt Pindi Chana amesema ili kuwa na misitu bora
nikuilinda na kuihifadhi ili kuziwezesha sekta nyingine kukua huku akiwaomba
askari hao kutumia silaha kwa utaratibu mzuri ili kulinda heshima ya jeshi la
uhifadhi.
"Ndugu viongozi na makamanda nyinyi nyote mnao wajibu wa
kulinda na kuendeleza rasilimali za misitu na nyuki,hili ni jukumu la msingi
ambalo mbinu za kijeshi zinatakiwa kuwezesha kufikia lengo hili yani kuwa na
misitu bora katika kuziwezesha sekta zingine kukua" amesema Dkt Pindi
chana.
Kwa upande wake Prof.Dos Santos Silayo Kamishna wa uhifadhi Wakala wa huduma za Misitu Tanzania(TFS) ameitaja changamoto ya kuongezeka kwa
matishio ya kiusalama na ongezeko la wananchi kujichukulia sheria mkononi jambo
ambalo linapelekea kujeruhiwa na kuuawa kwa baadhi ya askari na maafisa
wakati wakitekeleza majukumu yao.
"Ni changamoto kubwa sana na hizi siku za karibuni
matukio haya yamekuwa yakiongezeka, lakini kama jeshi la uhifadhi
tumejipanga katika kukomesha vitendo hivi,lakini pia kuongezeka kwa vyombo vya
usafiri hususani pikipiki katika maeneo ya uhifadhi nalo pia ni changamoto
kubwa sana,na changamoto hii tunaendelea kuifanyia kazi kwa kushirikiana na mamlaka
mbalimbali zinazosimamia vyombo hivi" amesema Prof silayo.
Hata hivyo dhamira ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) ni kuwa
na usimamizi endelevu wa rasilimali za kitaifa za misitu na nyuki ili kuchangia
mahitaji ya kijamii, kiuchumi, ki-ikolojia na kiutamaduni kwa kizazi cha sasa
na kijacho”.
Mwisho.
Comments
Post a Comment