Na Rhoda Simba, Dodoma
IMEBAINISHWA kuwa wagonjwa
wanaopelekwa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI)wengi wao ni wa ajali za pikipiki
maarufu bodaboda ambazo zimeonesha kuongoza kwa asilimia 70 na matibabu yake
kwa wagonjwa hao gharama ni kubwa kuanzia Shilingi milioni 1.5 na kufika hadi
shilingi Milioni 30.
Hayo yamebainishwa leo
jijini hapa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya mifupa Muhimbili
(MOI),Dkt.Respicous Boniface wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu
utekekezaji wa shughuli za taasisi hiyo na mwelekeo wa utekekezaji kwa mwaka wa
fedha 2022/23 ambapo amesema kumtibia mgonjwa mmoja ambaye amepata tatizo la
kuvunjika katika ajali ya bodaboda gharama zake ni kubwa.
Dkt.Boniface amesema Bodaboda
hufika MOI wamevunjika mifupa mikubwa wanaumia vichwa hasa ubongo na wengine
huwekwa muda mrefu wodi ya wagonjwa mahututi ICU.
“Kama Taasisi tumekuwa
tukiwahudumia wagonjwa hawa wa ajali za Bodaboda kwa aliyevunjika mfupa gharama
ni Shilingi milioni 1.5 lakini akiumia kichwa akakaa ICU gharama yake ni
Shilingi milioni tano hadi sita na akikaa miezi mitatu hapo gharama ndipo
inakuwa kubwa hadi kufikia Shilingi Milioni 30,
“Wagonjwa hawa wa ajali za
Bodaboda wengi hawana bima na wana hali za chini za kimaisha kwahiyo huwa ni
changamoto na kupelekea wengine kutelekezwa wodini na familia zao,”amesema.
Aidha amesema kuwa wagonjwa
wengine wengi ambao wamekuwa wakiwapokea ni watoto wenye vichwa vikubwa na
migongo wazi.
Akizungumzia utekelezaji wa
shughuli za taasisi hiyo na mwelekeo wake Dkt.Boniface amesema kuwa Huduma mpya
zilizoanzishwa MOI imeifanya Taasisi hiyo kuokoa fedha nyingi ikiwemo zaidi ya
shilingi milioni 608 ambazo zingetumika kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwajili
ya kuondoa uvimbe kwenye sakafu ya ubongo.
Ametaja huduma hizo kuwa ni ya
kuondoa uvimbe kwenye sakafu ya ubongo kupitia tundu la pua (transsphenoidal
hypophysectomy)ambapo Wagonjwa 19 wameshafanyiwa upasuaji na gharama za
upasuaji huo kwa hapa nchini ni shilingi milioni 8 na nje ya nchi ni Tshs
milioni 40 hivyo zingetumika kupeleka wagonjwa hawa nje ya nchi.
“Matumizi ya maabara ya Upasuaji
wa Ubongo (angio – suit curthlab)Katika kipindi hiki wagonjwa 186 wamehudumiwa
katika maaabara hii gharama za huduma hii hapa nchini ni kati ya Tsh milioni
5-10 na nje ya nchi ni Tsh million 30 mpaka 60 hivyo Taasisi imeokoa kati ya
Tsh bilioni 5.6 hadi Tsh bilioni 11.2 ambazo zingetumika
Pamoja na hayo amesema kuwa
Serikali imekuwa ikitoa fedha kwajili ya kununulia vifaa kwajili ya matibabu
ambapo imeshatoa Tsh Bilioni 4.4 kwajili ya ununuzi wa mashine mpya ya kisasa
ya MRI na CT scan kwa lengo la kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma hiyo kwa
uhakika.
“Taasisi imenunua vifaa vya
kisasa, zikiwemo,ICU Ventilators, Monitors, Vitanda na Ambulance ya kisasa
vyenye thamani ya tsh. billion 1.3 zilizotolewa na Serikali,”amesema.
Pia amesema Taasisi hiyo
imenunua vifaaa vya chumba cha tiba Mtandao vya shilingi milioni 227 kwa ajili
ya kuimarisha huduma hiyo nchini pamoja na Ununuzi wa Vipandikizi Serikali
imetoa kiasi cha shilingi 4.2 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa ‘Implants’ ili
kukabiliana na changamoto la uhaba wa implants kwa wagonjwa.
“Vifaa hivi vimesaidia kuendelea
kuboresha huduma za matibabu ya kibingwa ya Mifupa, Ubongo, Uti wa mgongo na
Mishipa ya Fahamu, na hivyo kuokoa maisha ya Watanzania wengi na pesa za
serikali ambazo zingetumika kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa matibabu Katika
kipindi hiki cha mwaka mmmoja jumla ya wagonjwa 7,113 walifanyiwa upasuaji
ikilinganishwa na wagonjwa 6,793 waliofanyiwa katika mwaka uliopita wa
2020/2021 ikiwa ni ongezeko la asilimia 2,”amesema Dkt.Boniface.
Mwisho.

Comments
Post a Comment