Na Muhammed
Khamis,TAMWA-ZNZ
Mkurugenzi wa Chama cha
Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA-ZNZ Dkt,Mzuri Issa amesema ili tuweze
kukuza usawa wa kijinsia visiwani Zanzibar kuna ulazima waandishi wa habari
kutoa taarifa za wanawake na maendeleo yao katika Nyanja tofauti zikiwemo
za uongozi, na maendeleo ya kijamii.
Amesema ili usawa wa
kijinsia upatikae ni lazima kuwe na mkakati maalumu wa kuwajenga waandishi wa
habari chipukizi ambao wataweza kutoa habari zinazohusus wanawake kwa ufanisi
mkubwa.
Aliyasema hayo wakati
akifungua mkutano wa siku moja wa kupitia mtaala maalumu utakaotumika
kufundishia waandishi wa habari vijana kupitia mradi wa kuwajengea uwezo
wanawake na uongozi kupitia vyombo vya habari.
‘’Kwa kuwa wanahabari ni
sauti ya wasio na sauti, kuwa kupitia mafunzo hayo maalumu yatakayowajengea
uwezo wanahabari vijana 18 kutoka Unguja na Pemba ninaamini kwamba
watakwenda kutatua tatizo la muda mrefu lililokosa wakulisemea na kuwafanya
wanawake wengi zaidi kushindwa kufikia malengo yao’’aliongezea.
Sambamba na hayo alisema
pia mafunzo hayo yatawajenga wanahabari waweze kuandika habari zenye
kuleta manufaa zaidi sambaba na kuwa wachambuzi wa mambo mbali mbali kupitia
maandiko yao au vipindi watakayotaarisha wakati wakiendelea na mafunzo yao ya
mwaka mmoja.
Awali akiwasilisha
ripoti ya mtaala utakaotumika kuwafundishia wanahabari hao vijana Mhadhiri
kutoka Chuo kikuu cha Taifa Zanzibar Dkt,Salum Sleiman Ali alisema wakati TAMWA-ZNZ
inajipanga kufanya mafunzo kwa wanahabari hao vijana hawana budi kuzingatia
yale yote yalio muhimu ambayo wanaamini yatawajengea uwezo wanahabari hao na
kuwafanya kuwa wadadisi.
Akibainisha miongoni mwa
vipengele muhimu ambavyo amependeleza kufundishwa ni pamoja na kuwajengea uwezo
wanahabari hao vijana katika kutengeneza habari bora na zenye kuleta mabadiliko
kwa jamii husika hususani kwa wanawake ambao ndio walengwa.
Baadhi ya wajumbe
wakichangia ripoti hiyo walisema ni jambo jema kuwajengea uwezo wanahabari na
walisema ni wajibu wa wale wote ambao watanufaika na mafunzo hayo kufanya kazi
kwa bidii kuonesha uwezo wao wa kuisaidia jamii ya wanawake.
Mhadhiri kutoka Chuo
kikuu cha Taifa Idara ya habari Imane Duwe alisema katika mafunzo hayo
wanahabari wanapaswa pia kufundishwa namna bora ya kujitegemea na
kujitolea zaidi kutokana na kuongezeka kwa wimbi kubwa la changamoto katika
upatikanaji wa ajira.
Alisema wanahabari
watakapofundishwa namna bora ya kuendesha kazi zao bila ya kuajiriwa wataweza
kuibua mengi mazuri kwa faida ya jamii kwa kuwa hawatakua na sehemu ambayo
watahofia kutoskilikana kwa kazi zao.
Nae msaidizi mhariri wa
shirika la magazeti ya Serikali Zanzibar Juma Khamis alisema ili kujenga kizazi
bora cha wanahabari watapaswa pia kufundishwa na kuzifahamu vyema kanuni za
maadili ya uandishi wa habari kwa lengo la kuepuka kujingiza kwenye matatizo
yanayoweza kuepukika.
Mradi wa kuwajengea
uwezo wanahabari vijana 18 Zanzibar unatekelezwa na TAMWA-ZNZ kwa kushirikiana
na shirika la The National Endowment
for Democracy (NED) kutoka Marekani.
Comments
Post a Comment