Imeelezwa kuwa, mradi wa ujenzi wa
njia ya kusafirisha umeme ya kV 400 kutoka Iringa-Tanzania hadi
nchini Zambia (TAZA) utaanza kutekelezwa Januari, 2023 na utakamilika Januari
2025 hali itakayopelekea kuimarika kwa upatikanaji umeme katika mikoa ya
Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe na Rukwa pamoja kuiwezesha Tanzania kufanya
biashara ya umeme katika nchi za kusini mwa Afrika na Afrika Mashariki.
Hayo yalielezwa tarehe 27 Julai,
2022 wakati Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba alipofika katika eneo
kutakapojengwa kituo cha kupoza na kukuza umeme cha Tunduma wilayani Momba,
Mkoa wa Songwe ambapo kituo hicho ni moja kati ya vituo vitano vya kupoza umeme
vitakavyojengwa kwenye mradi huo.
Mratibu wa Mradi wa TAZA, Mhandisi
Elias Makunga alisema kuwa mradi huo utatekelezwa kwa jumla ya shilingi
Trilioni 1.4 ambazo tayari Tanzania inazo na kwamba mradi utakuwa ni
kiunganishi cha kwanza cha umeme wa juu kati ya Nchi Wanachama wa Kusini mwaka
Afrika (SAPP) na Nchi Wanachama wa Mashariki mwa Afrika (EAPP) hali
itakayochagiza biashara ya umeme kwani Tanzania itaweza kununua umeme nje ya
nchi pale panapokuwa na upungufu na pia inaweza kuuza umeme nje ya nchi pale
inapokuwa na ziada.
Aliongeza kuwa, shilingi Bilioni
23.1 zimetengwa kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi zaidi ya 6,198
waliopisha mradi huo ambapo Wizara ya fedha kuanzia mwezi wa Nane mwaka
huu itafanya uhakiki ili kila mwananchi apate fidia stahiki kabla ya mradi
kuanza kutekelezwa.
Waziri wa Nishati, January Makamba
alisema kuwa mradi huo una muhimu wa kipekee kwani unaifanya Tanzania kuwa
kiungo cha biashara ya umeme katika nchi za Kusini mwa Afrika na Mashariki mwa
Afrika na pia mradi huo unaipa Tanzania nafasi ya kuendelea kuzalisha umeme
zaidi hata utakaozidi mahitaji ya nchi kwani kuna fursa pia za biashara ya
umeme.
“Tuna matumaini mradi utakamilika
ndani ya miaka miwili kwani umetengwa katika vipande Nane hivyo kutakuwa na
wakandarasi wengi watakaofanya kazi kwa kwa mpigo na hii itawezesha kujengwa
kwa vituo vitano vya kupoza umeme pamoja na njia ya kusafirisha umeme kutoka
Iringa hadi Rukwa pamoja na kipande cha kwenda mpaka wa Zambia.” Alisema
Makamba
Aidha, katika kutekeleza kipaumbele
cha Wizara ya Nishati cha kupeleka umeme kwenye maeneo ya uzalishaji ikiwepo
migodi, Waziri wa Nishati alifika katika Kijiji cha Itumbi, wilayani Chunya
Mkoa wa Mbeya ili kuzungumza na wachimbaji wadogo ambapo aliwaeleza
hatua zilizochukuliwa na Serikali za kupeleka umeme kwenye maeneo yao ya
uchimbaji, kusikiliza kero zao pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati safi
na salama ya kupikia.
Waziri wa Nishati aliwaeleza
wachimbaji hao kuwa, maeneo 22 ya uchimbaji madini wilayani humo yatapata umeme
kupitia mradi wa Gridi Mapato ambao tayari una shilingi bilioni 300
ambazo zitapeleka umeme kwenye maeneo ya uzalishaji ikiwemo migodi na viwanda
nchini.
Aliongeza kuwa, wakandarasi wa
kupeleka umeme kwenye migodi wilayani humo wataanza kazi mwezi wa 10 mwaka huu
na kwamba kazi ya kusambaza umeme kwenye maeneo mengine ya kijiji hicho
inaendelea baada ya kupata umeme takriban miezi mitatu iliyopita.
Katika hatua nyingine, Waziri wa
Nishati ameendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia ambapo
alitoa mitungi ya gesi kwa vikundi vya mamalishe ikiwa ni programu maalumu ya
majaribio ambayo itawezesha Serikali kupata taarifa zitakazozewesha kutengeneza
mpango mkubwa wa kitaifa wa usambazaji wa gesi nchini.
.jpg)
Comments
Post a Comment