Waziri wa Nishati, Mhe. Januari ametoa ufumbuzi wa changamoto ya miaka mingi ya mgawo wa umeme wa masaa 12 kwa vijiji 20 katika Wilaya ya Ludewa ambavyo vimekuwa vikipata umeme kutoka kampuni ya Madope.
![]() |
Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba akimsikiliza mmoja wa Wananchi katika Kijiji cha Lugarawa wilayani Ludewa baada ya kufika kijijini hapo kutatua changamoto ya upatikanaji umeme |
Kampuni hiyo ya Madope inayoendesha mradi huo mdogo wa umeme wa maji (MW
1.7 inaundwa na wadau mbalimbali wakiwemo Jumuiya ya Watumia Umeme
Lugarawa na Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa.
Changamoto hiyo ya mgawo wa umeme imetokana na waya unaotumika kusambaza
umeme kuwa mdogo ukilinganisha na mahitaji ya wananchi ambao wanaotumia umeme
kwa shughuli za kiuchumi kama vile kuendesha mashine za kukamulia alizeti na
kukoboa na kusaga nafaka.
Akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Lugarawa wilayani humo, Waziri
Makamba amesema kuwa, Serikali kupitia TANESCO imeamua kununua umeme wote
unaozalishwa na kampuni hiyo baada ya kufanya mazungumzo na wadau wote
wanaohusika na mradi huo pamoja na TANESCO.
Amesema kuwa, kwa TANESCO kununua umeme huo kutawezesha wananchi kupata
umeme wa uhakika kwani kwa sasa katika megawati 1.7 zinazozalishwa, umeme
unaotumika ni 0.3 na pia kampuni hiyo ya Madope itapata mapato.
Ameongeza kuwa, Wataalam wa TANESCO watafika Lugarawa tarehe 7 Agosti
2022 ili kufanya tathmini ya Miundombinu ya Usafirishaji umeme pamoja na
kusaini mikataba ya makubaliano hayo na inategemewa kuwa ifikapo mwezi wa
Pili mwaka 2023 wananchi hao watakuwa wameshaanza kupata umeme wa uhakika.
Mradi huo wenye wateja 3200 kwa sasa umeleta manufaa mbalimbali kwa
wananchi wa Kijiji hicho ikiwemo kutoa huduma ya umeme katika vituo vya afya,
shule za Sekondari 5, shule za msingi 19 na kituo kimoja cha kulelea watoto
yatima.
Utekelezaji wa Mradi wa umeme wa Madope umewezeshwa na wadau mbalimbali
ikiwemo Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambao ulitoa shilingi Bilioni 4.5
kuendeleza mradi huo.
Wananchi pamoja na viongozi katika Wilaya hiyo akiwemo Mbunge wa
Ludewa,, Mhe. Joseph Kamonga wamemshukuru Waziri wa Nishati kwa kutoa ufumbuzi
wa changamoto hiyo ambayo imedumu kwa muda mrefu.
Akiwa wilayani humo Waziri wa Nishati ameendelea kuhamasisha matumizi ya
nishati safi na salama ya kupikia ambapo ametoa mitungi ya gesi kwa kinamama
ikiwa ni mradi wa majaribio utakaofanyiwa tathmini ili Serikali itengeneze
mkakati bora wa kitaifa wa namna bora ya kusambaza nishati hiyo nchini.
Comments
Post a Comment