Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WENYEVITI na wakurugenzi wa halmashauri nchini
wametakiwa kuichambua bajeti iliyopitishwa na serikali ili wananchi katika
ngazi za chini wawe na uelewa na kunufaika nayo.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), Murshid Ngeze |
Agizo hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala
za Mitaa Tanzania (ALAT), Murshid Ngeze alipokuwa akiongea katika Mkutano wa
mwaka wa ALAT tawi la Mkoa wa Dodoma uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa
Halmashauri ya Jiji la Dodoma mwishoni mwa wiki.
Ngeze alisema kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa
na Rais Samia Suluhu Hassan imepitisha bajeti ya kihistoria na ya mfano. “Ndugu
zangu, bajeti hiyo imejaa fursa mbalimbali zenye manufaa kwa halmashauri zetu
na wananchi wetu. Wenyeviti wote na wakurugenzi wa halmashauri ni wajibu wenu
kuichambua bajeti hiyo na kuwaeleza wananchi ili fedha zitakapokuja kwenye
halmashauri zetu ziweze kuwanufaisha na sisi kuzisimamia ipasavyo” alisema
Ngeze.
Aidha, aliwataarifu wajumbe kuwa Mkoa wa Kagera
umepata shilingi bilioni 70 kwa ajili ya kuanzisha ufugaji wa samaki kwa njia
ya vizimba. Alishauri kuwa Mkoa wa Dodoma kujipanga kwa ufugaji huo kutokana na
kutokuwa na bahari wala ziwa. Ufugaji huo ni wa kawaida na hauhitaji uwekezaji
mkubwa, aliongeza.
Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Dodoma, Zuberi White |
Awali akimkaribisha Mwenyekiti wa ALAT Taifa,
Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Dodoma, Zuberi White alisema kuwa ALAT Mkoa wa
Dodoma ni wamoja na wanafanya kazi kwa ushirikiano.
Mkutano wa mwaka wa ALAT Mkoa wa Dodoma ulifanyika
katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ukitanguliwa na ziara ya siku moja ya
kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa jijini hapo.
MWISHO
Comments
Post a Comment