Na Mwandishi Maaum – Dar es Salaam
WATAALAMU 20 kutoka Taasisi ya Moyo Uganda wametembelea Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam kwaajili ya kuona huduma za
matibabu ya moyo zinatolewa pamoja na kujifunza namna ambavyo taasisi hiyo
inavyoendesha shughuli zake.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi amesema baada ya kusikia
mafanikio yaliyopatikana katika Taasisi hiyo wataalamu hao kutoka nchini Uganda
wameona ni vyema kwenda kujifunza mafanikio hayo pamoja na changamoto zake ili
nao wafikie hatua kama ya JKCI.
Prof.Janabi
amesema tangu Taasisi hiyo ianzishwe mwaka 2016 imekuwa na mafanikio makubwa
katika utoaji wa huduma za matibabu ya moyo kwa kufanya upasuaji kwa wagonjwa
8663 na kuona wagonjwa zaidi ya laki sita na hivyo kuwa hospitali bora ya
Serikali inayotoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo katika nchi za
Afrika Mashariki na Kati.
“Mwaka
2017 baadhi ya wabunge kutoka nchini Uganda walitembelea Taasisi yetu kwa ajili
ya kujifunza na leo hii tumepokea wataalamu 20 kutoka nchini humo ambao nao
wamekuja kujifunza jinsi tulivyofanikiwa katika utoaji wa huduma za matibabu ya
moyo. Sisi tumefanikiwa kwa kuwa Serikali inatuunga mkono kwa zaidi ya asilimia
120 na hata upasuaji tunaoufanya ni salama”,.
“Taasisi
yetu inapokea wagonjwa kutoka nchi za Afrika ya Mashariki na Kati ikiwemo
Uganda ambapo kwa mwaka huu tumeshafanya upasuaji wa moyo kwa watoto sita
ambao walikuwa na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo. Watoto hawa wanaendelea
vizuri na walisharudi nchini mwao”, amesema Prof. Janabi.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Prof. William Mahalu alisema amefurahi kuona wenzao kutoka nchini Uganda
wamekuja kuwatembelea kwaajili ya kujifunza wanachokifanya na na
kuwaeleza walipofikia ili wawasaidie kutokana na mapungufu waliyokuwa nayo.
“Ukiangalia
historia ya kuanzishwa kwa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete haitofautiani na ya
kuanzishwa kwa Taasisi ya Moyo Uganda kwani zote zimetokea katika Hospitali
za Taifa, jambo la muhimu ni kuwatia moyo ili wasikate tamaa na kuweza
kufika hapa tulipofika sisi kwani wao wako hatua tatu nyuma yetu”.
Prof.
Mahalu ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu
alisema Taasisi ya Moyo Uganda ni ya Serikali, kwani huduma za matibabu
ya moyo bila kushikiliwa na Serikali zinagharama kubwa na zikiwa na utashi wa
kisiasa kuwa zinawasadia watu wataweza kupata kila kitu ambacho
watakitaka na hivyo kuweza kufanya vizuri katika kutoa huduma kwa wagonjwa.
Dkt.
James Magara ambaye ni Mwenyekiti wa bodi ya Taasisi ya Moyo Uganda alisema
wamekuja nchini kujifunza katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ili wasifanye
makosa kiutendaji kwani wao wako katika hatua za mwanzo tangu taasisi hiyo
ianzishwe na kama wataanza vizuri wataweza kufanya vizuri zaidi.
“Tanzania
na Uganda tumekuwa na mahusiano mazuri tangu miaka ya nyuma, tumefaidika
na Tanzania kwani wakati wa vita vya Idd Amin Tanzania ilikuja kutusaidia. Na
sisi leo tumekuja kujifunza kwa wataalamu wenzetu kuona ni vitu gani
wamevifanya na kuweza kufikia hatua hii kwani kuwa na Taasisi kama JKCI siyo
kitu cha muda mfupi”, alisema Dkt. Magara.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Uganda Dkt. John Omagino alisema
Serikali ya nchi hiyo imeamua kujenga kituo cha matibabu ya moyo ili kupunguza
idadi ya wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi. Pia kituo hicho kiwe na ubora
sawa na vituo vingine vya Afrika Mashariki ili wagonjwa wa moyo watibiwe
ndani ya nchi hizo ikiwemo Uganda.
Dkt.
Omagino alisema taasisi yao bado ni ndogo na wanatakiwa kusonga mbele
zaidi, Serikali yao imewapa ardhi na wamepata fedha ambazo zitawawezesha
kujenga jengo kubwa la Taasisi hiyo hivyo basi ili waweze kufanya kitu kizuri
wameona watembelee vituo vingine vya moyo vilivyopo Afrika Mashariki na
kujifunza vitu ambavyo vimewafanya wamefanikiwa hii ikiwa ni pamoja na
kusomesha wataalamu wa afya.
“Gharama
za matibabu ya moyo ni kubwa na wengi wanashindwa kulipia lakini wenzetu
wa JKCI wanatoa huduma kwa watu wote wa kipato cha juu, cha kati na cha chini
tumekuja kuona ni jinsi gani wamefanikiwa katika hili”,.
“Changamoto
tunayokutana nayo ni namna ya kuwasomesha wataalamu nje ya nchi kwani wengine
wanaenda kusoma muda mrefu zaidi ya miaka mitano na wengine hawarudi pindi
wanapomaliza masomo yao, lakini kama tutakuwa na kozi za muda mfupi ndani ya
nchi zitatusaidia watalamu hawa wakimaliza masomo yao wataendelea na kazi ndani
ya nchi yao”, Dkt. Omagino .
Dkt.
Omagino alisema wanaangalia jinsi gani ya kuzuia magonjwa hayo na siyo
kutibu kwani kama watu watafuata mtindo bora wa maisha wataepukana na magonjwa
ya moyo hii ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi, kula vyakula bora, kupunguza
unywaji wa pombe uliokithiri na kuacha matumizi ya tumbaku.
Wataalamu
hao ambao ni wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Uganda wameambatana na watunga
sheria na sera watakuwa katika Taasisi hiyo kwa muda wa siku mbili na
watatembelea maeneo mbalimbali ya JKCI pamoja na kuzunguma za wakuu wa Idara
ili waweze kubadilishana ujuzi wa kazi.
Mwisho
Comments
Post a Comment