Simbachawene: Makundi ya watu wenye ulemavu yashirikishwe katika mchakato mzima wa Sensa ya Watu na Makazi
Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
Serikali imesema itaendelea kuyashirikisha makundi ya watu wenye
ulemavu katika hatua mbalimbali za
maandalizi na utekelezaji wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linalo tarajiwa
kufanyika Agosti 23,2022.
Hayo yamesemwa Juni 29,2022 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na
Uratibu George Simbachawene katika kongamano la kuwajengea uelewa watu wenye
ulemavu kuhusu Sensa ya Watu na Makazi .
‘’Ushirikishwaji wa kundi la Watu Wenye Ulemavu katika
mchakato mzima wa Sensa umesaidia sana katika kuimarisha maswali ya hali ya
ulemavu katika Sensa, hivyo matarajio ya Serikali ni kupata takwimu bora za
hali ya ulemavu katika kaya zetu ili hatimae kusaidia utungaji Sera na upangaji
wa mipango na programu za maendeleo zinazogusa Watu Wenye Ulemavu kwa uhakika
zaidi kuliko ilivyo hivi sasa.’’ amesema Simbachawene
Aidha, Simbachawene amesema kumekuwepo na jitihada mbalimbali
za kuimarisha ukusanyaji wa takwimu za Watu Wenye Ulemavu na taasisi mbalimbali
zimeonesha nia ya kufanya tafiti za kupata idadi na hali ya Watu Wenye Ulemavu
ili kuelewa mahitaji yao halisi kwa lengo la kuboresha hali zao za maisha.
‘’Takwimu za Watu Wenye Ulemavu ni muhimu sana kwa kuwa ni msingi mmojawapo sio tu wa kuhakikisha ustawi wa Watu Wenye Ulemavu nchini bali pia ni utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kuleta maendeleo jumuishi nchini.’’ ameongeza Simbachawene
Wakati huo huo, amesema upatikanaji wa takwimu sahihi za
msingi za Watu Wenye Ulemavu zitawezesha kutunga sera wakilishi na kusaidia kupima
utekelezaji wa malengo mbalimbali ya kitaifa, kikanda na kimataifa .
‘’Kama vile Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP
III) na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) ambayo yote imeweka mkazo katika
kuhakikisha Watu Wenye Ulemavu sio tu wanakuwa sehemu ya mipango ya maendeleo
ya nchi bali wanapewa kila fursa za kujiendeleza katika nyanja zote za maendeleo
kama wananchi wengine.’’ amesema Simbachawene
Katika hatua nyingine, Simabachawene ameiagiza Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania
Bara, na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Tanzania Zanzibar kuendelea
kuboresha mbinu za ukusanyaji wa taarifa hizi za hali ya ulemavu nchini,kushirikiana
na taasisi mbalimbali zinazojihusisha na Watu Wenye Ulemavu kwa lengo la kuwatambua
na kuwahudumia.
‘’Sambamba na kuendelea kutoa msaada wa kitaalamu kwa vyama
mbalimbali vya Watu Wenye Ulemavu katika kuwajengea uwezo wa kukusanya taarifa
za hali ya ulemavu nchini.’’ ameongeza Simbachawene
Hatahivyo , amesema Ofisi za takwimu ziendelee kujumuisha
maswali yanayolenga kupata taarifa za hali ya ulemavu nchini kwenye tafiti
mbalimbali zinazofanywa na Ofisi hizo.
Mwisho.
Comments
Post a Comment