Na. Dennis Gondwe, DODOMA
JUMUIYA ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) imeipongeza
Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa umakini wake katika kuwasilisha michango kwa
wakati jambo linaloonesha nia njema na uwajibikaji unaolenga kuifanikisha
taasisi hiyo.
Mwenyekiti wa ALAT Taifa, Murshid Ngeze |
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa ALAT Taifa,
Murshid Ngeze alipokuwa akiongea katika Mkutano wa mwaka wa ALAT tawi la Mkoa
wa Dodoma uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la
Dodoma mwishoni mwa wiki.
Ngeze alisema “niishukuru Halmashauri ya Jiji la
Dodoma, katika michango ya ALAT Taifa. Halmashauri hii ndiyo inaongoza ulipaji
wa michango kwa wakati. Nilipokutana na Waziri wa TAMISEMI nilimshauri kumuacha
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma ili aendelee kutekeleza mipango mizuri aliyonayo
kwa Jiji la Dodoma na miradi ya maendeleo”.
Aidha, aliipongeza ALAT tawi la Mkoa wa Dodoma kwa
kazi nzuri. “Sasa umefika wakati ALAT Mkoa wa Dodoma kufikiria kuanzisha miradi
ya kiuchumi ili tuache alama. Tufikirie miradi itakayoisaidia ALAT kuwa na mapato
ya uhakika na kuachana na kutegemea mapato ya kuombaomba” alisema Ngeze.
Mwenyekiti huyo alielezea masikitiko yake kwenye
halmashauri zenye migogoro na kusema kuwa inakwamisha maendeleo ya wananchi.
“Mheshimiwa Rais anaona na kusikitishwa na migogoro katika halmashauri.
Ameiagiza ALAT kuondoa migogoro hiyo na kuhakikisha halmashauri zinachapa kazi.
Hadi sasa kuna halmashauri zipo kwenye migogoro ya kumuondoa Meya na mwenyekiti
wa halmashauri, jambo linalochelewesha maendeleo ya wananchi” alisema Ngeze.
Awali akimkaribisha Mwenyekiti wa ALAT Taifa,
Mwenyekiti wa ALAT mkoa wa Dodoma, Zuberi White alisema kuwa ALAT Mkoa wa
Dodoma ni wamoja na wanafanya kazi kwa ushirikiano.
Mkutano wa mwaka wa ALAT Mkoa wa Dodoma ulifanyika
katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ukitanguliwa na ziara ya siku moja ya
kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa jijini hapo.
MWISHO
Comments
Post a Comment