Na Gaspary Charles- TAMWA ZNZ
MKURUGENZI Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania,
Zanzibar (TAMWA ZNZ), Dkt. Mzuri Issa amesema jamii iliyo na uwezo wa kutambua
mapungufu na kubaini changamoto zinazokwamisha upatikanaji wa haki zao ndio
msingi wa ufikiwaji fursa sawa za kimaendeleo kwa njia ya kidemokrasia katika
jamii.
Alieleza kuwa jamii nyingi zinakabiliwa na matatizo mbalimbali
yanayokwamisha haki na maendeleo yao lakini zinashindwa kuyatatua kutokana na
kukosa uwezo thabiti wa kuyazungumzia katika ngazi husika ili kufanyiwa kazi
kwa wakati.
Dkt. Mzuri alieleza hayo wakati akizungumza na wahamasishaji
Jamii kudai haki zao na wanawake kushiriki katika masuala ya uongozi na
demokrasia Pemba kupitia mradi wa kushajihisha wanawake katika uongozi
unaotekelezwa kwa mashirikiano ya TAMWA ZNZ, Jumuiya ya Wanasheria Wanawake
Zanzibar (ZAFELA) na jumuiya ya Utetezi wa Mazingira na Jinsia Pemba (PEGAO)
kwa ufadhili wa Ubalozi wa Norway Nchini.
Alifahamisha kwamba iwapo jamii itakuwa na uwezo wa kuyaibua
matatizo yanayowakabili na kuchukua hatua sahihi itasaidia kuchochea
uwajibikaji katika upatikanaji wa haki zao.
Mapema mkurugenzi huyo alihimiza wahamasishaji jamii hao ambao
wanafanya kazi katika Wilaya zote nne za Micheweni, Wete, Mkoani na Chake Chake
kisiwani Pemba kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kuwasaidia wananchi kuwa na
uwezo wa kuibua matatizo yanayowakabili na kuyataftia ufumbuzi kwenye vyombo
husika.
“Dhana ya mradi kuunda wahamasishaji jamii ni kuhakikisha
yule mwananchi wa chini awe na uwezo wa kuyaibua matatizo yanayomkabili, kisha
aweze kuchukua hatua dhidi ya matatizo hayo na kuwa na ujasiri wa kukaa meza
moja na mamlaka husika kutafta ufumbuzi kwa njia ya demokrasia,” alisema Mzuri.
Aidha alieleza kuwa uwepo wa wahamasishaji hao katika jamii
unalenga kuwafanya watoa huduma wa taasisi mbalimbali kuongeza kasi ya
uwajibikaji dhidi ya utatuzi wa vikwazo vinavyowakabili wananchi kwenye maeneo
yao.
Alieleza, “majukumu makubwa ya wahamasishaji jamii ni kuwafanya
watoa huduma wafanye kazi zao vizuri kwa uwazi, na wawajibike kwa wananchi
ipasavyo, na huo ndio msingi haswa wa dhana ya utawaka bora.”
Kutokana na wanawake kukosa misingi imara ya uelewa katika
masuala mbalimbali yatakayowajenga kwenye nafasi za uongozi, aliagiza
wahamasishaji hao kuangalia uwiano wa usawa wa kijinsia ndani ya kamati za
shehia ili kutoa fursa sawa kwa wanawake kutokana na huko ndipo msingi wa
uongozi unapoanzia.
Akiwasilisha ripoti ya uhamasishaji jamii kudai haki zao, Ali
Othman ambaye ni mhamasishaji jamii Wilaya ya Micheweni, alieleza kupitia
mikutano iliyofanyika kwenye shehia mbalimbali walibaini kuwepo baadhi
changamoto ikiwemo uelewa mdogo wa wanawake katika masuala yatakayowasaidia
kuingia kwenye nafasi za uongozi jambo ambalo linakwamisha ushiriki wao
kikamilifu katika nafasi hizo.
Aidha alibainisha changamoto nyingine ni uwepo wa vyeti feki vya
kuzaliwa kwa baadhi ya wananchi wa Shehia ya Shumba, Wilaya ya Micheweni mkoa
wa Kaskazini Pemba, jambo ambalo linapelekea wananchi wengi kukosa haki zao za
msingi ikiwemo nafasi za uongozi.
“Tatizo la uwepo wa vyeti feki vya kuzaliwa kwa wakaazi wa
Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba ni moja ya changamoto kubwa
tuliyoibua kwenye jamii, kwani katika mikutano yetu kwenye shehia wananchi
wengi hasa Shehia ya Shumba Mjini kilio chao ilikuwa ni kupata vyeti feki,”
alieleza mhamasishaji huyo.
Aidha alifahamisha kuwa uwepo wa wahamasishaji hao katika jamii
umesaidia kujenga uwezo kwa jamii kuwa na uthubutu wa kuzungumza matatizo
yanayowakabili kwa uwazi.
Nae Husna Khamis kutoka Wilaya ya Wete alieleza, baada ya
kubaini kuwepo kwa tatizo la kutojua kusoma na kuandika kwa wananchi wengi hasa
wanawake, walishirikiana na jamii kuanzisha madarasa ya watu wazima ili
kuwapatia fursa wananchi kuondokana na tatizo hilo linalowakosesha haki zao
muhimu.
Alisema, “kupitia uhamasishaji kwenye shehia, tumefanikiwa
kuzindua madarasa 6 ya watu wazima yakiwa na jumla ya watu 130 kwaajili ya
kuwawezesha kusoma na kuandika katika Shehia ya Mlindo, Wilaya ya Wete na
tayari wengi wao wameshaanza kujua kusoma na kuandika.”
Mapema afisa tathimini na ufuatiliaji wa ZAFELA, Rajab Hamad,
alipongeza juhudi zinazochukuliwa na wahamasishaji hao kwa kufanikisha
ufuatiliaji wa changamoto na vikwazo vinavyo chelewesha upatikanaji wa haki za
wananchi.
“Niwapongeze sana wahamasishaji jamii Pemba kwa kufanikisha
ufuatiliaji wa changamoto za wananchi na kuhakikisha zote tulizofuatilia
zinakuwa na matokeo chanya kutokana na ufuatiliaji mliofanya kwenye ngazi
mbalimbali, na hii ni kwasababu kwamba lengo la mradi huu wa SWIL sio tu kuibua
matatizo ya wananchi ila ni kusaidia kushirikiana na jamii kutafta ufumbuzi wa
matatizo hayo.”
Mradi wa kushajihisha ushiriki wa wanawake katika uongozi
na demokrasia ni mradi wenye lengo la kukuza ushiriki wa wanawake katika
uongozi ambao unatekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake
Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar
(ZAFELA) na jumuiya ya Utetezi wa Mazingira na Jinsia Pemba (PEGAO) kwa
ufadhili wa Ubalozi wa Norway Nchini.
----------------------------------------MWISHO-----
Comments
Post a Comment