ALAT MKOA WA DODOMA YAPANDISHA KIWANGO CHA ELIMU

Na. Dennis Gondwe, DODOMA

JUMUIYA ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) Mkoa wa Dodoma inajivunia kupandisha kiwango cha ufaulu katika mkoa kutoka nafasi ya 23 mwaka jana kwa elimu ya sekondari.

Zuberi White


Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) Mkoa wa Dodoma, Zuberi White alipokuwa akifungua mkutano wa mwaka wa ALAT mkoa uliofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

White alisema “ALAT Mkoa wa Dodoma tumetekeleza kwa asilimia 90. Vikao vyetu vyote vimefanyika kwa mujibu wa ratiba. Kwa upande wa elimu ya sekondari, Mkoa wa Dodoma tumepanda sana. Dodoma tulikuwa nafasi ya 23, ila mwaka tumepanda sana na kukosa pointi moja kuingia 10 bora. Hongera kwa wenyeviti na wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Dodoma kwa kazi nzuri”.

Mwenyekiti huyo aliwashauri wajumbe kuihamasisha jamii ili watoto wasome. “Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutupatia fedha za mapambano dhidi ya UVIKO-19. Mheshimiwa Rais ametusaidia sana katika kukamilisha madarasa. Wanafunzi wote wamepelekwa shule na hatukuwa na chaguo la pili msimu huo” alisema White.

Aidha, aliwakumbusha kuwa uchumi na maendeleo ni mambo yanayokwenda pamoja na kuwasisitiza kuinua uchumi wa wananchi wao. “Karibuni Dodoma makao makuu ya nchi. Niwahakikishie ni salama kwa watu wote” alisisitiza White.

Mkutano wa mwaka wa ALAT Mkoa wa Dodoma ulifanyika katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ukitanguliwa na ziara ya siku moja ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa jijini hapo.

 

MWISHO

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.