Na. Moses Mpunga, DODOMA
Watumishi wa
serikali mkoani Dodoma wamemshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha maslahi ya watumishi wa
Umma kwa kupandisha mishahara kwa asilimia 23.3 pamoja na posho mbalimbali.
Shukrani hizo zilitolewa na
Mtunza Kumbukumbu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Imelda Matofali katika hafla fupi ya kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa kuboresha maslahi ya watumishi katika ukumbi wa mikutano wa PSSSF
jijini hapa.
Matofali
akizungumza kwa niaba ya watunza kumbukumbu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma, alimshukuru Rais kwa kuwakumbuka watumishi wa kada za chini. Alisema
kuwa Rais amewakumbuka kwa kuwaongezea mishahara pamoja na posho jambo ambalo
halikuwahi kufanyika kwa muda mrefu. "Kama mnavyojua Rais wetu ni mama na
sifa kubwa ya mama ni kuwakumbuka watoto wake. Hivyo, tunamshukuru sana mama
kwa kutukumbuka na sisi tunamuahidi kuchapa kazi kwa nguvu zetu zote"
alisema Matofali.
Akiwawakilisha
Watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Afisa Mtendaji Kata ya Uhuru,
Christina Mpete alimuhakikishia Rais Samia Suluhu Hassan kuwa watumishi
wataongeza juhudi katika kufanya kazi na kuwa atembee kifua mbele wao wapo
nyuma yake na hawatamuangusha. Alisema kuwa ongezeko hilo la mishahara na posho
limeongeza morali ndani ya watumishi wa Halmashauri hiyo.
"Mama yetu
tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu akulinde na akupe afya njema ili uendelee
kuchapa kazi na kutuhudumia watanzania" aliongeza Mpete.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Mkoa wa Dodoma, Mwl. Samweli Malechela alisema
licha ya kuongeza mishahara na posho, Rais amelipa malimbikizo mengi ya
mishahara kwa watumishi ndani ya mwezi uliopita. Katika Mkoa wa Dodoma, walimu
zaidi ya 2,300 walipandishwa madaraja.
Mwl. Malechela
aliongeza kuwa kupanda kwa mishahara na posho kutaimarisha na kuboresha uchumi
wa watumishi pamoja na watanzania kwa ujumla. Mzunguko wa fedha utakua ni
mkubwa jambo litakalopelekea uchumi wa Taifa kukua pia, aliongeza.
"Licha ya
mambo yote ya kuboresha maslahi ya watumishi anayoyafanya Mama Rais wetu
mpendwa lakini bado miradi mikubwa inaendelea kwa kasi ileile. Kwahiyo, ni
dhahiri kabisa kuwa mama anaupiga mwingi. Hivyo, ni jukumu letu kumuunga mkono
kwa kufanya kazi kwa juhudi kubwa ili kuendena na kauli ya kazi iendelee"
alimalizia Mwl. Malechela.
MWISHO
Comments
Post a Comment