WANANCHI DODOMA WASHAURIWA KULIMA ZABIBU

Na. Mwandishi wetu, DODOMA

Wakazi wa Kata ya Zuzu katika Wilaya ya Dodoma wametakiwa kulima Zabibu kwa sababu ni zao la kimkakati katika wilaya hiyo litakalowaletea maendeleo ya kiuchumi.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri


Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alipofanya ziara ya kikazi kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika kata ya Zuzu iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Shekimweri aliwaomba wananchi kushiriki katika kilimo cha zao la Zabibu ambalo ni zao la kimkakati wilayani Dodoma. “Ndugu zangu, nawaomba sana kushiriki katika kilimo cha Zabibu kwa sababu ni zao la kimkakati” alisema Shekimweri.

Aidha, aliwataka wananchi hao kuunga mkono juhudi za serikali za kuwaletea maendeleo. Alisema kuwa wapo baadhi ya watu wenye nia ovu wanaopinga na kushawishi wengine kupinga juhudi za serikali kuwaletea maendeleo kwa kutoa taarifa za upotoshaji.

Akiongelea Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, aliwataka wananchi hao kujitokeza kuhesabiwa ifikapo tarehe 23 Agosti, 2022. Sensa ni muhimu kwa serikali kupanga mipango ya maendeleo na uboreshaji wa huduma za kijamii, aliongeza.

Katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya aliambatana na Kamati ya Usalama ya wilaya, maafisa kutoka Wakala wa Barabara vijijini (TARURA), Mthamini wa Mkoa na maafisa kilimo wa Halmashauri.

 

 

MWISHO

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.