Wananchi 437 wamefanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo na kisukari ambapo asilimia 60 wamekutwa na matatizo

 Na. Mwandishi Maalum – Chalinze, Pwani

30/05/2022 Wananchi 437 wamefanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo na kisukari ambapo asilimia 60 wamekutwa na tatizo la shinikizo la juu la damu (Presha) na asilimia 20 ya waliokutwa na tatizo hilo tayari walishapata madhara ya shinikizo la juu la damu ikiwa ni pamoja na moyo kutokufanya kazi vizuri na kutanuka kwa misuli ya damu ya moyo.

Afisa kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Aliston Jovin akiwagawia vipeperushi vinavyoelezea huduma za matibabu zinazotolewa na JKCI wananchi waliofika katika Hospitali ya Halmashauri ya Chalinze iliyopo Msoga kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo uliofanywa na wataalam wa moyo kutoka JKCI katika Halmashauri hiyo iliyopo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani


Wananchi wengine walikutwa na matatizo ya matundu kwenye moyo, mishipa ya damu ya moyo kutokukaa katika mpangilio wake, matatizo kwenye vyumba vya moyo na mishipa ya damu ya moyo kushindwa kupitisha damu vizuri.

Hayo yamesemwa jana na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Peter Kisenge wakati wa kufanya tathimini ya zoezi la upimaji wa magonjwa ya moyo na kisukari lililofanyika katika hospitali ya Halmashauri ya Chalinze iliyopo Msoga wilayani Bagamoyo.

Dkt. Kisenge ambaye pia ni mkuu wa kitengo cha mafunzo na utafiti wa Taasisi hiyo alisema wagonjwa 27 walikutwa na matatizo ya moyo yaliyohitaji uchunguzi na matibabu ya kibingwa na hivyo kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.

“Katika upimaji huu tulifanya upimaji kwa watoto 22 ambapo watatu kati yao walikutwa na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu ya moyo kutokuwa katika mpangilio wake wa kawaida, watoto hawa tumewapa rufaa ya kuja kufanyiwa kufanyiwa uchunguzi zaidi na kutibiwa katika Taasisi yetu”,.

“Zoezi la upimaji limeenda vizuri mwitikio ni mkubwa wananchi wamekuja kwa wingi na wamefurahia kupata matibabu kutoka kwa wataalamu wetu. Kwa kuwa tatizo la shinikizo la juu la damu ni kubwa nawashauri wananchi waepuke uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe uliopitiliza na kutokula vyakula vyenye mafuta mengi pia wazingatie lishe bora na ufanyaji wa mazoezi kwa kufanya hivi wataepuka kupata magonjwa ya moyo”, alisema Dkt. Kisenge.

Dkt. Kisenge alisema Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete inaunga mkono jitihada za Serikali za kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma za matibabu ya kibingwa kwa kuwafuata wananchi mahali walipo kwa ajili ya kutoa huduma za upimaji wa magonjwa ya moyo na kisukari bila malipo yoyote yale kwa kufanya hivi wananchi wengi wataweza kufikiwa na huduma za matibabu ya kibingwa ya magonjwa hayo kwa haraka zaidi.

Afisa Uuguzi kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Rahabu Tamba akimpima urefu na uzito mwananchi aliyefika katika Hospitali ya Halmshauri ya Chalinze iliyopo Msoga wilayani Bagamoyo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo uliokua ukifanywa na wataalam wa moyo kutoka JKCI kwa wananchi wa Chalinze


Naye Mganga mkuu wa Halmashauri ya Chalinze Dkt. Allen Mlekwa  aliwashukuru wataalamu waliotoa huduma za upimaji na matibabu kwa wananchi na kusema upimaji huo ulihusisha madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa JKCI pamoja na wenzao wa Hospitali ya Msoga.

Dkt. Mlekwa alisema waliokutwa na matatizo ya  moyo wengine walikuwa na kliniki katika hospitali mbalimbali na walikuwa wanatumia dawa lakini waliacha kutokana na sababu mbalimbali na baada ya kufanyiwa vipimo vya moyo wamekutwa mioyo yao imetanuka na wengine wamekutwa na ugonjwa sugu wa kisukari. Baadhi yao hawakuwa wanafahamu kabisa kuwa na tatizo la moyo na hivyo waliwaanzishia dawa za kutumia.

“Kuwepo kwa zoezi hili la upimaji kumetufanya tufahamu kunatatizo kubwa la watu wenye matatizo ya moyo na kisukari  hivyo basi nasi tumejipanga kuboresha kliniki yetu ya moyo na kisukari iliyopo katika Hospitali ya Msoga kwa siku ya alhamisi ili wagonjwa waliokuwa wanakwenda kutibiwa Hospitali za Tumbi, Amana, Mwananyamala na Muhimbili waje kutibiwa hapa”,.

“Kwa kuwa tuna mashine za kupima vipimo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO) na kuchunguza mfumo wa umeme wa moyo (Electrocardiography - ECG) tutawafanyia wagonjwa wenye shida ya moyo vipimo hivi hapa hapa na kama tutawakuta na matatizo makubwa tutawarufaa kwenda kutibiwa katika Hospitali kubwa zaidi”,.

“Wananchi wengine wametoka kilomita zaidi ya 100 karibu kabisa  na Tanga na Mvumero wamekuja hapa kwa ajili ya kufuata huduma hii ya upimaji, tutajipanga ili tuweze kufanya mobile kliniki za kwenda kutoa huduma za upimaji katika vituo vya afya vya Msata, Kibindu, Lugoba na Miono kwa kufanya hivi wananchi wengi watafikiwa na huduma za matibabu ya moyo na kisukari”, alisema Dkt. Mlekwa.

Kwa upande wa wananchi waliopata huduma hiyo walishukuru kwa huduma ya uchunguzi na matibabu ya bila malipo  waliyoipata na kusema imewapunguzia gharama ya kusafiri na kuwafuata wataalamu Dar es Salaam pamoja na kulipia matibabu hayo.

Fredrin Ikumbera mkazi wa Lugoba alisema alipima vipimo na kukutwa moyo uko sawa lakini amekutwa na shida ya presha amepewada dawa za kutumia pamoja na  ushauri wa lishe bora na kuambiwa apunguze matumizi ya vyakula vya wanga pamoja kupunguza kunywa pombe kwani ni hatari kwa afya ya moyo wake.

“Nilikuwa ninawasiwasi kuhusu moyo wangu kwani mazingira niliyokuwa naishi hayakuwa salama. Ninawasihi wananchi wenzangu kutumia  nafasi za upimaji pindi zinapotokea kwa kwenda kupima afya zao pia kwa upande wa Serikali iendelee kuhakikisha wananchi walioko vijijini wanapata huduma za matibabu ya kibingwa kwani kutokana na mazingira yao ni vigumu kufikiwa na huduma hizi”, alisema Ikumbera.

Mwisho

 

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.