Wananchi 437 wamefanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo na kisukari ambapo asilimia 60 wamekutwa na matatizo
Na
Mwandishi Maalum – Chalinze, Pwani
30/05/2022 Wananchi
437 wamefanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo na kisukari ambapo asilimia
60 wamekutwa na tatizo la shinikizo la juu la damu (Presha) na
asilimia 20 ya waliokutwa na tatizo hilo tayari walishapata madhara ya
shinikizo la juu la damu ikiwa ni pamoja na moyo kutokufanya kazi vizuri na
kutanuka kwa misuli ya damu ya moyo.
Wananchi wengine walikutwa na matatizo ya matundu kwenye moyo,
mishipa ya damu ya moyo kutokukaa katika mpangilio wake, matatizo kwenye vyumba
vya moyo na mishipa ya damu ya moyo kushindwa kupitisha damu vizuri.
Hayo yamesemwa jana na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Peter Kisenge wakati wa kufanya tathimini
ya zoezi la upimaji wa magonjwa ya moyo na kisukari lililofanyika katika
hospitali ya Halmashauri ya Chalinze iliyopo Msoga wilayani Bagamoyo.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni mkuu wa kitengo cha mafunzo na
utafiti wa Taasisi hiyo alisema wagonjwa 27 walikutwa na matatizo ya moyo
yaliyohitaji uchunguzi na matibabu ya kibingwa na hivyo kupewa rufaa ya kwenda
kutibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.
“Katika upimaji huu tulifanya upimaji kwa watoto 22 ambapo
watatu kati yao walikutwa na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni
matundu na mishipa ya damu ya moyo kutokuwa katika mpangilio wake wa kawaida,
watoto hawa tumewapa rufaa ya kuja kufanyiwa kufanyiwa uchunguzi zaidi na
kutibiwa katika Taasisi yetu”,.
“Zoezi la upimaji limeenda vizuri mwitikio ni mkubwa wananchi
wamekuja kwa wingi na wamefurahia kupata matibabu kutoka kwa wataalamu wetu.
Kwa kuwa tatizo la shinikizo la juu la damu ni kubwa nawashauri wananchi
waepuke uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe uliopitiliza na kutokula vyakula
vyenye mafuta mengi pia wazingatie lishe bora na ufanyaji wa mazoezi kwa
kufanya hivi wataepuka kupata magonjwa ya moyo”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete inaunga
mkono jitihada za Serikali za kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma za
matibabu ya kibingwa kwa kuwafuata wananchi mahali walipo kwa ajili ya kutoa
huduma za upimaji wa magonjwa ya moyo na kisukari bila malipo yoyote yale kwa
kufanya hivi wananchi wengi wataweza kufikiwa na huduma za matibabu ya kibingwa
ya magonjwa hayo kwa haraka zaidi.
Naye Mganga mkuu wa Halmashauri ya Chalinze Dkt. Allen Mlekwa
aliwashukuru wataalamu waliotoa huduma za upimaji na matibabu kwa
wananchi na kusema upimaji huo ulihusisha madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo
wa JKCI pamoja na wenzao wa Hospitali ya Msoga.
Dkt. Mlekwa alisema waliokutwa na matatizo ya moyo wengine
walikuwa na kliniki katika hospitali mbalimbali na walikuwa wanatumia dawa
lakini waliacha kutokana na sababu mbalimbali na baada ya kufanyiwa vipimo vya
moyo wamekutwa mioyo yao imetanuka na wengine wamekutwa na ugonjwa sugu wa
kisukari. Baadhi yao hawakuwa wanafahamu kabisa kuwa na tatizo la moyo na hivyo
waliwaanzishia dawa za kutumia.
“Kuwepo kwa zoezi hili la upimaji kumetufanya tufahamu
kunatatizo kubwa la watu wenye matatizo ya moyo na kisukari hivyo basi
nasi tumejipanga kuboresha kliniki yetu ya moyo na kisukari iliyopo katika
Hospitali ya Msoga kwa siku ya alhamisi ili wagonjwa waliokuwa wanakwenda
kutibiwa Hospitali za Tumbi, Amana, Mwananyamala na Muhimbili waje kutibiwa
hapa”,.
“Kwa kuwa tuna mashine za kupima vipimo vya kuangalia jinsi moyo
unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO) na kuchunguza mfumo wa umeme wa moyo
(Electrocardiography - ECG) tutawafanyia wagonjwa wenye shida ya moyo vipimo
hivi hapa hapa na kama tutawakuta na matatizo makubwa tutawarufaa kwenda
kutibiwa katika Hospitali kubwa zaidi”,.
“Wananchi wengine wametoka kilomita zaidi ya 100 karibu kabisa
na Tanga na Mvumero wamekuja hapa kwa ajili ya kufuata huduma hii ya
upimaji, tutajipanga ili tuweze kufanya mobile kliniki za kwenda kutoa huduma
za upimaji katika vituo vya afya vya Msata, Kibindu, Lugoba na Miono kwa
kufanya hivi wananchi wengi watafikiwa na huduma za matibabu ya moyo na
kisukari”, alisema Dkt. Mlekwa.
Kwa upande wa wananchi waliopata huduma hiyo walishukuru kwa
huduma ya uchunguzi na matibabu ya bila malipo waliyoipata na kusema
imewapunguzia gharama ya kusafiri na kuwafuata wataalamu Dar es Salaam pamoja
na kulipia matibabu hayo.
Fredrin Ikumbera mkazi wa Lugoba alisema alipima vipimo na
kukutwa moyo uko sawa lakini amekutwa na shida ya presha amepewada dawa za
kutumia pamoja na ushauri wa lishe bora na kuambiwa apunguze matumizi ya
vyakula vya wanga pamoja kupunguza kunywa pombe kwani ni hatari kwa afya ya
moyo wake.
“Nilikuwa ninawasiwasi kuhusu moyo wangu kwani mazingira
niliyokuwa naishi hayakuwa salama. Ninawasihi wananchi wenzangu kutumia
nafasi za upimaji pindi zinapotokea kwa kwenda kupima afya zao pia kwa
upande wa Serikali iendelee kuhakikisha wananchi walioko vijijini wanapata
huduma za matibabu ya kibingwa kwani kutokana na mazingira yao ni vigumu
kufikiwa na huduma hizi”, alisema Ikumbera.
Mwisho
Comments
Post a Comment