WALIMU 258,291 NA WADAU WENGINE KUNUFAIKA NA TOVUTI MPYA YA TUME BAADA YA WADAU WA AWALI 182,650 KUNUFAIKA NA ILE YA AWALI
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Prof. Willy Lazaro
Komba, leo katika Mkutano wa Tume amezindua tovuti mpya ya TSC inayotarajiwa
kuhudumia Walimu wapatao 258,291 ambao ni Walimu 173,591 wa Shule za Msingi na
Walimu 84,700 wa Sekondari tofauti na Wadau mbalimbali 182,650 walionufaika na
tovuti ya awali iliyokua na changamoto kadhaa.

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Prof. Willy Lazaro Komba
Akiongea na washiriki wa hafla ya uzinduzi huo iliyofanyika Jijini
Dodona katika Ukumbi wa Chama cha Mapinduzi (Jakaya Kikwete Convention Center)
alisema pamoja na kuhudumia walimu, hao tovuti mpya itawahudumia pia wadau
wengine wote wa Sekta ya Elimu, Taasisi, Wananchi na Taifa kwa
ujumla.
Prof.Komba alisema, “Kwa kipindi cha miaka saba sasa (2017 - 2022) tangu
Tume kuwa na tovuti, taarifa na mambo mbalimbali ya TSC ambayo Tume ingependa
yawafikie walengwa na jamii kwa ujumla kwa wakati tarajiwa ili kufikia malengo
ya utekelezaji zimekua haziwafikii kama ilivyotarajiwa kutokana na changamoto
za hapa na pale zilizobainishwa ikiwemo changamoto ya mabadiliko makubwa ya
kiteknolojia duniani katika eneo la Habari, Elimu, Mawasiliano na Uhamasishaji.
Aidha, kabla ya kuzindua tovuti hiyo; aliwaelekeza na kuwasisitiza
Maafisa TEHAMA na Mawasiliano ya Serikali katika uendeshaji wa tovuti pamoja na
zana nyingine zote za mawasiliano na jamii, uhabarishaji, uelimishaji na
uhamasishaji ikiwemo mitandao ya jamii, kuzingatia viwango, maelekezo na
miongozo yote ya Serikali kwani pamoja na kufuata maelekezo hayo wamewezeshwa
kwa mafunzo kuwa na umiliki wa moja kwa moja wa zana hizo za mawasiliano hali
inayosababisha uhuishaji wa taarifa na kufanya maboresho mbalimbali kwa wakati
kuwa rahisi.
Hali kadhalika, Prof. Komba alisema kuwa ni matumaini yake kuanzia sasa
taarifa zote hai zenye tija kwa Walimu, Wateja, Wadau na Jamii kwa ujumla wake
zitapatikana kwa wakati zikiwa hai na zenye tija kwa walengwa ikiwa ni pamoja
na kuwezesha wateja kupata huduma muhimu za Tume kupitia tovuti hiyo mpya bila
kulazimika kutembelea Ofisi za Tume Makao Makuu au katika Ofisi za Tume ngazi
ya Wilaya zote 139.
“Imeelezwa hapa kuwa tovuti mpya iliyoboreshwa itakuwa chanzo sahihi na
bora kwa Walimu, Wateja na Wadau mbalimbali wa Sekta ya Elimu kupata taarifa
mbalimbali za Tume. Ni wazi taarifa na maudhui yatakayowekwa kwenye tovuti
yatatumika kwa usahihi katika kazi mbalimbali ikiwemo kujifunza, kufanya
tafiti, kupata huduma na rejea ya nyaraka mbalimbali kuhusu masuala ya Utumishi
wa Walimu. Nawasihi wadau wote hususan walimu kuitumia tovuti hii kupata
huduma, taarifa, maudhui, takwimu na nyaraka mbalimbali kwa rejea na matumizi
sahihi.” Alisema Mwenyekiti huyo wa TSC.
Aliwashukuru wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine katika
kufanikisha zoezi la kutengeneza tovuti hiyo iliyogharimu Tzs.6,000,000/=
wakiwemo Wadau wa Maendeleo ambao alisema ndiyo msaada na chanzo cha awali cha
kuifanikisha Tume kuwa na tovuti, na kipekee aliwashukuru sana Makamishna wa
Tume kwa ushirikiano wao, Wajumbe wa Menejimenti ya TSC kwa utekelezaji kwa
wakati, vilevile Kamati ya TEHAMA ya Tume kwa maoni na ushauri wao, na Idara na
Vitengo vyote kwa kuwezesha mchakato wa kumpata mzabuni wa kutekeleza kazi hiyo
ikiwa ni pamoja na kuandaa maudhui na taarifa mbalimbali ambazo zitatumika
kwenye tovuti hii.
Kwa namna ya pekee Prof. Komba alivipongeza Kitengo cha TEHAMA na
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali vya Tume kwa uratibu wa zoezi zima la
matengenezo ya tovuti hiyo kwa pamoja na Watalaam wa TEHAMA kutoka Ofisi ya
Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Wizara ya Fedha na
Mipango (MoFP) na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwa ushauri na kazi kubwa
ya kutengeneza tovuti na kuwapa mafunzo Maafisa Watalaam wa Tume.
Nae Katibu wa Tume, Mwl. Paulina Nkwama, kabla ya kumkaribisha
Mwenyekiti wa Tume, Prof. Willy Komba, alizitaja baadhi ya changamoto
zilizopelekea maelekezo ya Tume kwa Menejimenti ya Tume kutengenezeza tovuti
mpya kuwa ni pamoja na; tovuti ya awali kutengenezwa kwa teknolojia ya zamani,
waendeshaji tovuti kutokuwa na uelewa wa kutosha kwenye masuala ya usimamizi wa
tovuti hiyo, uhitaji mkubwa wa kuboresha mwonekano na maudhui ya
tovuti, uelewa hafifu na usio fasaha wa namna ya kuandaa na kupandisha taarifa,
takwimu na nyaraka mbalimbali kwenye tovuti, Maafisa TEHAMA, Habari na
Mawasiliano kutokuwa na umiliki wa moja kwa moja (ownership) hali ambayo
ilisababisha changamoto katika kuhuisha taarifa na kufanya maboresho mbalimbali
kwa wakati, na tovuti kutokidhi mahitaji ya Tume kwa kutokuwa na maeneo ya
kutosha kwa ajili ya kuweka taarifa mbalimbali za Taasisi.
Katibu huyo alisema, “Tofauti na tovuti ya awali, tovuti hii mpya ni
bora zaidi kwa kuwa; inakidhi mahitaji ya Tume kutokana na uwezo wake wa kubeba
taarifa nyingi zaidi kwa wakati mmoja, inaendana na teknolojia ya kisasa, ina
uwezo mkubwa wa kuingiza na kupokea maudhui na maboresho ya taarifa kwa wakati,
Maafisa wa TSC (TEHAMA na Mawasiliano ya Serikali) kupitia mafunzo yaliyotolewa
wana uelewa wa kutosha katika usimamizi (administration) na uendeshaji, na
tovuti hii inamsaidia mtumiaji (Walimu na wadau wengine wa Tume) kupata
viunganishi (links) vya mifumo mingine mbalimbali kwa urahisi.”
Akiwasilisha taarifa ya mwenendo wa tovuti ya Tume kabla ya uzinduzi
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali wa Tume, Gerard Chami, alisema
pamoja na faida zilizoainishwa huduma na vitu vitakavyopatikana katika tovuti
hiyo mpya ni pamoja na; Ufahamu wa Majukumu ya Tume kwa mujibu wa Sheria
iliyoanzisha Tume, Sheria ya Tume na Kanuni zake, maelezo na taratibu za
upatikanaji wa huduma mbalimbali zitolewazo na Tume, machapisho mbalimbali
ikiwemo Miongozo, Mipango Mkakati, Tafiti, Taarifa, Sera, Majarida, Takwimu,
Fomu mbalimbali za mtandaoni katika Utumishi wa Umma, na eneo la habari ambamo
kutakua na Taarifa mbalimbali kwa Vyombo vya Habari, Hotuba, Vipeperushi,
Vibango, Vibonzo, habari picha mnato, habari picha jongefu, Mawasiliano ya Tume
pamoja na ramani mtandao ya kufika Ofisi za Tume Makao Makuu, Dodoma na Ofisi
za Wilayani zote 139.
Chami alisema vile tovuti mpya iliyoboreshwa itakuwa ni chanzo sahihi na
bora cha taarifa mbalimbali kuhusu Tume kwa Walimu, Wananchi, Wadau wa Elimu na
Taasisi mbalimbali, Kitengo cha TEHAMA kimejipanga vema kusimamia kikamilifu
tovuti hiyo ili iweze kufanya kazi na kupatikana kwa muda wote huku Kitengo cha
Mawasiliano ya Serikali nacho kikiahidi kuhuisha taarifa kwa wakati na kwa
kadri zinavyohitajika kwa walaji ili wadau wote waweze kupata taarifa kwa
wakati na waweze kutumia huduma zilizopo kwenye tovuti hiyo.
Kamishna Assela Luena akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Makamu
Mwenyekiti wa Tume, Kamishna Bahati Mgongolwa, alisema kukamilika kwa tovuti
mpya ni jambo la kheri, lenye tija na manufaa makubwa kwa Tume na Taifa kwa
ujumla wake kwani inaenda kuhudumia sehemu kubwa zaidi ya wateja wa TSC hususan
Walimu, Wadau wa Elimu, Watafiti, Taasisi mbalimbali za Umma na Binafsi pamoja
na Wananchi kwa ujumla na kupunguza uhaba wa awali wa upatikanaji wa taarifa
mbalimbali muhimu kwa wateja wa Tume.
Hafla hiyo ya uzinduzi wa tovuti mpya ya Tume ulihudhuriwa na
Waheshimiwa Makamishna wa Tume, Katibu wa Tume, Wajumbe wa Menejimenti ya Tume,
Wajumbe wa Kamati ya TEHAMA ya Tume, Mtaalamu mwakilishi kutoka Mamlaka ya
Serikali Mtandao (e-GA), Sekretarieti ya Mkutano wa Tume, Wanahabari na
Watumishi wa Tume.
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Prof. Willy Komba akitoa
hotuba katika hafla ya uzinduzi wa tovuti mpya ya TSC iliofanyika katika Ukumbi
wa Mikutano wa Jakaya Kiwete jijini Dodoma, Mei 27, 2022.
Comments
Post a Comment