Mratibu wa TAMWA Zanzibar ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said |
JUMLA ya kesi 39 za udhalilishaji
wa kijinsia katika wilaya za Mkoani na Wete Pemba zimeibuliwa na mtandao wa
kupinga udhalilishaji wa wilaya hizo katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari
hadi mei mwaka huu.
Wakiwasilisha ripoti ya ufuatiliaji
wa matukio hayo katika jamii kwa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake
Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) wanamtandao hao wameeleza kuwepo kwa
mitandao ya kupinga udhalilishaji katika jamii kumesaidia kuongeza hamasa kwa wanajamii
kuwa tayari kujitokeza kuripoti taarifa za matukio ya kesi za udhalilishaji wa
kijinsia jambo ambalo limechochea uchukuaji wa hatua dhidi ya matukio hayo
katika ngazi mbalimbali.
Mwenyekiti wa mtandao huo wilaya ya
Mkoani, Haji Shoka alisema katika utekelezaji wa majukumu ya mtandao huo
wamefanikiwa kufuatilia kesi kumi kwenye wilaya hiyo ambazo zipo
katika hatua mbalimbali.
“Kuanzia mwezi Januari hadi Mei kwa
wilaya ya Mkoani tumeibua kesi kumi za udhalilishaji ambapo kati ya kesi hizo,
kesi nne zipo kwenye vituo vya polisi zikiendelea na upelelezi, kesi nne zipo
mahakamani na kesi moja mtuhumiwa katoroka na nyingine moja imesuluhishwa
nyumbani,” alieleza mwenyekiti huyo.
Aidha alieleza kutokana juhudi za
mitandao hiyo kufanya mikutano ya uelimishaji jamii kwenye jamii juu ya
kupambana na vitendo hivyo, hatua hiyo imesaidia kubadili mitazamo ya wanajamii
kupunguza usuluhishi wa kesi hizo majumbani.
Alifahamisha, katika kutekeleza
kazi zetu, mtandao umefanikiwa sana katika mambo mawili, kwanza jamii nyingi
zimeanza kubadilika na wanaripoti matukio ya kesi za udhalilishaji katika
sehemu husika tofauti na zamani ambapo walikuwa wanaripotiu kwa sheha na
kupelekea kesi nyingi kusuluhishwa katika ngazi ya familia jambo ambalo
lilipelekea wahanga wa matukio haya kuathirika zaidi kisaikolojia.”
Aidha alibainisha kuwa katika
kipindi hicho mtandao ulifanya mikutano ya utoaji elimu ya udhalilishaji kwa
watoto kupitia skuli na madrasa ikiwa na lengo la kuwatayarisha watoto kutambua
viashiria vya udhalilishaji na namna ya kujikinga navyo.
Alisema, “kwa mwaka huu pia
tuliendelea na zoezi la utoaji wa elimu katika maeneo mbalimbali ambapo
tumetembelea madrasa na skuli mbalimbali na jumla ya watu 1,374 kati yao
wanawake 748, na wanaume 626 tumewafikia.”
Nae Siti Faki Ali, mwenyekiti wa
mtandao huo Wilaya ya Wete alisema kwa upande wa wilaya hiyo walifuatilia na
kuibua kesi 29 ambapo kati ya hizo kesi za ubakaji zilikuwa 14.
“Katika wilaya ya Wete tumefanikiwa
kufuatilia na kuibua jumla ya kesi 29, kesi za ubakaji zikiwa ni kesi 14,
kutorosha sita, shambulio la aibu nne, kunajisi mvulana nne, kumpa mimba mwari
kesi moja ambapo kati ya hizo, kesi 20 zinaendelea na upelelezim na hakuna kesi
iliyotolewa hukumu kwa kipindi hiki,” Siti Faki ali, mwanamtandao,” alieleza.
Akizungumzia kuhusu utoaji wa elimu
ya udhalilishaji mwenyekiti huyo alibainisha kwamba Jumla ya watu 2,115
walifikiwa na elimu hiyo kati yao wanawake wakiwa ni 1,270 na wanaume 845.
Mapema mratibu wa TAMWA Zanzibar
ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said aliwataka wanamitandao hiyo kuendelea
kufikisha elimu kwenye jamii ili kuisaidia kuwa na taaluma ya kutosha ya
kujilinda dhidi ya matukio hayo.
“Wanamtandao tuna jukumu kubwa sana
la kusaidia wananchi kujua namna ya kutafuta na kupata haki zao hasa matukio
haya ya udhalilishaji, na huu ni wajibu wetu kwa pamoja kuhakikisha tunawalinda
wanawake na watoto dhidi ya matukio yote ya udhalilishaji katika jamii,”
alisema Fat-hiya.
Mkutano huo wa uwasilishaji ripoti
ya utekelezaji wa majukumu ya mtandao wa kupinga udhalilishaji Pemba ni sehemu
ya utekelezaji mradi wa kutumia jukwaa la Habari kumaliza vitendi vya
udhalilishaji wa Kijinsia unaotekelezwa na TAMWA ZNZ kwa kushirikiana na
Shirika la kimataifa la maendeleo la Denmark (DANIDA).
Comments
Post a Comment