WIZARA YATOA RAI KWA WADAU WA SEKTA YA UTALII NCHINI KUENDELEZA PROGRAMU YA ROYAL TOUR, YAGAWA VIFAA VYA KUJIKINGA NA UVIKO -19

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Francis Michael ameeleza kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea kushirikiana vizuri na wadau wa Sekta ya Utalii katika kuendeleza Programu ya Royal Tour ili kuvutia watalii kutoka katika masoko mbalimbali  duniani waje kutembelea vivutio vya utalii vya Tanzania.

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Francis Michael

Amesema Programu ya Royal Tour iliyozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan  ni fursa ya Kimkakati ya kuitambulisha Tanzania Kimataifa,kuvutia uwekezaji nchini na kutangaza utalii.

 

Dkt. Francis Michael ameyasema hayo leo jijini Arusha alipokuwa akigawa vifaa vya kujikinga na janga la UVIKO- 19 kwa Wadau wa Sekta ya Utalii nchini.

 

Amesema Sekta ya Utalii nchini Tanzania inaendelea kuimarika baada ya athari za janga la UVIKO 19  kutokana na jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuirejesha katika hali yake ya awali.

 

" Kipekee namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kutokana na jitihada mahususi alizozichukua za kuitangaza Tanzania Kimataifa kupitia programu maalum ya Royal Tour ambayo imeenda sambamba na kuimarisha mapambano dhidi ya UVIKO -19, ni ukweli usiopingika kuwa Royal Tour ni fursa ya kimkakati ya kuitambulisha Tanzania Kimataifa, kuvutia uwekezaji  na kutangaza utalii" Amesisitiza Dkt. Francis Michael.

 

Ameongeza kuwa katika Mapambano dhidi ya Janga la UVIKO -19, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kupitia Mpango wa Maendeleo aliipatia Wizara ya Maliasili na Utalii fedha shilingi Bilioni 90.2 ambapo sehemu ya fedha hizo zimetumika kuimarisha Sekta ya Utalii katika maeneo mbalimbali.

 

Ameyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa barabara zenye urefu wa  Kilometa 2,383.12 katika maeneo ya Hifadhi za Taifa, kujenga malango 14 ya kupokelea wageni katika maeneo ya hifadhi, Mapori ya Akiba, Tengefu na Misitu ya Hifadhi ya Mazingira Asilia.

 

Ameongeza kuwa  Wizara imetenga maeneo ya uwekezaji na uendelezaji wa shughuli za utalii, kutoa mafunzo katika Sekta ya Utalii na Tasnia ya Ukarimu kwa wadau wa Utalii nchini, kuimarisha ulinzi na usalama wa watalii katika maeneo ya vivutio na kuboresha mazingira ya biashara ikiwemo kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma mbalimbali.

 

Dkt. Francis Michael amebainisha kuwa taarifa za mwenendo wa Utalii zinaonesha kuwa katika kipindi cha msimu wa watalii mwaka huu Tanzania inatarajiwa kupokea idadi kubwa ya watalii na kuongeza kuwa matarajio hayo yanapaswa kwenda sambamba na maandalizi stahiki ya kupokea watalii hao na kuchukua tahadhari dhidi ya UVIKO -19.

 

Amesema kwa kutambua umuhimu huo Serikali imegawa imegawa vifaa vya kujikinga na janga la UVIKO -19 kwa wadau hao kupitia vyama vidogo vya watalii 10 vinavyojumuisha wafanyabiashara wadogo wadogo 16,056 ili kuhakikisha afya za wananchi na watalii zinalindwa ipasavyo na kuendelea kujenga imani kwa watalii kuwa Tanzania ni nchi salama ya kutembelewa.

 

Vifaa hivyo vinajumuisha barakoa 140,000 na vitakasa mikono 14,285.

 


Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.