Na Rhoda Simba Dodoma.
SERIKALI ya awamu ya sita chini
ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu
Hassan imedhamiria kuona haki za watumishi wa umma zinaendelea
kuboreshwa kadri Serikali itakavyokuwa na uwezo wa kifedha kufanya hivyo.
Aidha sambamba na
upandishwaji vyeo, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imepanga kuongeza
mishahara kuanzia asilimia 23.3 katika kima cha chini cha mshahara kwa mwezi
ili kuwapa nafuu watumishi wake kumudu gharama za maisha.
Hayo yamesemwa leo Mei 26 jijini
hapa na Waziri wa Nchi,ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
utawala bora Jenista Mhagma wakati akiufungua mkutano wa wakuu wa idara za
utawala na rasilimali watu katika utumishi wa umma ambapo amesema kuwa pamoja
na kazi nzuri ambayo inaendelea kufanywa, Utumishi wa Umma unakabiliwa na
changamoto mbalimbali zikiwemo za kushuka kwa uadilifu wa kazi katika utumishi
wa umma.
"Ninapozungumzia uadilifu
ninamaanisha masuala yote yanayohusu nidhamu, kushuka kwa weledi, ubadhirifu,
kutozingatiwa kwa Sheria, Kanuni, Taratibu na miongozo iliyopo katika
kushughulikia masuala mbalimbali ya kiutumishi na Menejimenti ya
rasilimaliwatu,’’amesema.
Amesema, kuwa mafanikio
yanayopatikana katika Nyanja za kiuchumi na kijamii yanaonesha weledi na ubunifu
mkubwa unaofanywa na watumishi wa umma huku Serikali ikijivunia huduma bora
zinazotolewa na watumishi wa umma zikiwemo ujenzi wa miundombinu ambayo
imesanifiwa na kusimamiwa na watumishi wa umma ikiwemo mifumo ya TEHAMA kama
vile Mfumo mpya wa Taarifa za Watumishi wa Umma na Mishahara (NEW HCMIS),
Miradi mikubwa ya Kitaifa ikiwemo ya Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) na Mradi wa
Uzalishaji wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP).
Amesema kuwa Serikali inatambua
kuwa wajibu wa wafanyakazi wa umma ni lazima uendane na haki zao kwa sababu
hiyo, kama sehemu ya kutekeleza wajibu wake katika mwaka wa fedha 2021/2022
Serikali kupitia Ofisi hiyo ilitoa vibali vya kuwapandisha madaraja watumishi
wa umma 92,619.
‘’Ni matarajio yangu kuwa,
watumishi wenye sifa wamepandishwa madaraja na baada ya zoezi hilo ninadiriki
kusema kuwa, kwa kiasi kikubwa malalamiko ya watumishi wenye sifa kutopandishwa
vyeo yatakuwa yamepungua kama siyo kuisha. Kabla ya hatua hiyo, Ofisi yangu
imekuwa ikipokea malalamiko mengi kutoka kwa watumishi kuhusu kutopandishwa
madaraja,’’amesema Mhagama.
Amesema kuwa Ofisi hiyo
itaendelea kufanya uchambuzi wa malalamiko yanayowasilishwa na watumishi wa
umma na Taasisi itakayobainika kuwa na watumishi wengi wenye malalamiko ambayo
yanatakiwa kutolewa majibu na mwajiri; Mwajiri na Mkuu wa Idara ya Utawala na
Utumishi wa Taasisi hiyo watakuwa wameshindwa kutekeleza majukumu yao, na hatua
stahiki zitachukuliwa dhidi yao kwa kuzingatia mamlaka yao ya nidhamu.
" Ninapenda kuwakumbusha
maelekezo ya Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa Watumishi wa Umma na
kwenu kama wasimamizi wa Rasilimaliwatu aliyoyatoa tarehe 21 Mei, 2022 wakati
akimwapisha Mwenyekiti na Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma,
''Mheshimiwa Rais amesistiza
kuhusu nidhamu ya kazi na uwajibikaji wa hiari kutoka katika nafsi zetu badala
ya kuonesha nidhamu pale panapokuwa na vitisho, Mheshimiwa Rais Samia
Suluhu Hassan alisema wakati watumishi wa umma wanapofurahia haki wanazopewa na mwajiri kama vile upandishwaji vyeo na nyongeza za mishahara wasisahahu
kutimiza wajibu wao wa kufanyakazi kwa kuzingatia maadili ya kazi zao, kwani
haki huenda na wajibu,’’amesisitiza Waziri.
Mwisho.

Comments
Post a Comment