DKT. JAFO: UHIFADHI WA MAZINGIRA NI JUKUMU LA KILA MMOJA

 


DODOMA.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Seleman Jafo amesema takriban kiasi cha hekta laki nne( 469,420) za misitu huharibiwa kila mwaka.

 

Pia, utupaji holela wa taka pamoja na  uwepo wa athari za mabadiliko ya tabianchi yamekuwa ni changamoto kubwa hapa nchini.

 

Waziri Jafo, ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma wakati akitoa tamko la serikali kuhusu maadhimisho ya siku ya Mazingira Duniani , amesema hali hiyo imekuwa ikiathiri maisha ya viumbe mbalimbali ikiwemo mifumo ya ikolojia ambapo hadi sasa imeliletea Taifa hasara takriban asilimia 5% ya pato la Taifa.

 

‘’Kutokana na hali hii, hivyo maadhimisho ya Siku ya Mazingira yaendelee kuwa chachu ya  kuongeza  kasi ya uhamasishaji  wa jamii  kushiriki shughuli za kuhifadhi na kutunza mazingira nchini.’’  amesema Dkt. Jafo

 

Wakati huo huo, Waziri Jafo ameitaka Mikoa yote kutumia radio za Halmashauri za mikoa kuhamasishana na kuelimisha jamii masuala yahusuyo hifadhi ya mazingira ikiwemo kutumia nishati mbadala wa mkaa majiko banifu pamoja na kutumia njia sahihi za kuhifadhi taka.

 

‘’Tukumbuke kwamba, suala la hifadhi ya mazingira ni jukumu letu sote na tunapaswa kulitekeleza kwa vitendo.’’amesisitiza Dkt. Jafo

 

Mbali na hilo, amesema watanzania wanapaswa kufahamu kuwa utunzaji na uhifadhi wa mazingira ni jumkumu la kila mmoja kwa nafasi yake kwakuwa wasipo tunza mazingira hakuna mtu kutoka sehemu nyingine kuja kufanya kazi hiyo.  

 

Pamoja na hayo , amesema Waziri Mkuu Kasim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika  kilele cha maadhimisho hayo ambapo atazindua Mpango Kabambe wa Kitaifa wa Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira. Mpango huo umebainisha changamoto za mazingira kuanzia ngazi ya mamlaka za Serikali za Mitaa, Mikoa pamoja na mifumo ikolojia mahsusi nchini.

 

‘’Mpango kabambe huo umetoa mapendekezo ya hatua za kukabiliana na changamoto husika kuendana na mahitaji ya kila eneo. Kwa muktadha huo, Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira utakuwa  ndio nyenzo muhimu katika kutoa muongozo wa kuandaa na kutekeleza miradi na programu za kuhifadhi mazingira nchini.’’ ameongeza Dkt. Jafo

 

Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kitaifa yatafikia kilele chake tarehe 5 Juni, 2021, Katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete kilichopo jijini Dodoma yakiongozwa na kauli mbiu isemayo ‘’Tanzania ni moja tu: Tutunze Mazingira’’

 

   

 

 

 


Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.