NA. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma kupeleka timu ya hamasa
na elimu juu ya Anuani za Makazi Kata ya Mbabala ili kufanikisha zoezi hilo.
Mkurugenzi wa Jiji, Joseph Mafuru |
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph
Mafuru alipokuwa akijibu swali la Diwani wa Kata ya Mbabala, Paskazia Mayala
aliyetaka kujua lini kata yake itapata uhamasishaji na wakazi wa kata hiyo
kupata namba za makazi katika nyumba zao jana katika mkutano wa Baraza la Madiwani
lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mkurugenzi Mafuru alisema kuwa elimu ya Anuani za Makazi
ilitolewa kwenye ngazi zote katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma. “Tulipeleka waratibu
kwenda kujifunza Morogoro. Waliporudi tukatoa elimu katika ngazi ya jiji,
watendaji na wenyeviti wa mitaa. Lengo lilikuwa kujua nani anaendesha zoezi hilo
na taratibu zake zilivyo ili kuwa na uelewa wa pamoja” alisema Mafuru.
Diwani wa Mbabala, Paskazia Mayala |
Akiongelea wataalam kwenda tena Kata ya Mbabala,
alisema kuwa watakwenda kesho (leo). “Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie kuwa
kesho wataalam wa Anuani za Makazi watafika Kata ya Mbabala na kufanya
uhamasishaji. Sasa hivi wanarudia kuhakikisha maeneo ambayo hawakufanya vizuri.
Mimi naangalia taarifa za kila siku za mwenendo wa zoezi hili. Kesho watakuwepo
Mbabala na kazi itafanyika kwa kiwango cha juu” alisema Mafuru kwa kujiamini.
Zoezi la uandikishaji Anuani za Makazi katika
Halmashauri ya Jiji la Dodoma limefikia asilimia 82.3.
MWISHO
Comments
Post a Comment