Wagonjwa
20 wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wa kufungua kifua katika kambi maalum
iliyofanywa na madaktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa
kushirikiana na daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kutoka
hospitali ya Max iliyopo nchini India na kumalizika jana Jijini Dar es Salaam.
Kambi
hii maalum ya matibabu ya moyo iliyoanza tarehe 18 hadi 25 Aprili 2022 imefanyika
kwa wagonjwa ambao mioyo yao ilikua imechoka na kiwango cha ufanyaji kazi wa
moyo umeshuka chini ya asilimia 35%.
Akizungumzia
kambi hiyo Mkurugenzi Idara ya Upasuaji JKCI Dkt. Angela Muhozya amesema kuwa
wagonjwa 7 (saba) wamefanyiwa upasuaji wa kubadilisha mshipa mkubwa wa moyo
(Aorta) uliokuwa umetanuka zaidi ya sentimita 5 (5cm)na hivyo kuwa katika
hatari ya kupasuka wakati wowote na mgonjwa kupoteza Maisha.
“Upasuaji
huu hufanyika kwa kuondoa sehemu iliyotanuka na kupandikiza kipande cha mshipa
wa bandia (graft) inayoendana na ukubwa wa mshipa wa moyo wa mgonjwa (ascending
aorta replacement) ambapo wagonjwa wote wanaendelea na matibabu na afya zao
zinazidi kuimarika”, alisema Dkt. Angela
Aidha
Dkt. Angela amesema kuwa pamoja na wagonjwa hao saba waliobadlilishiwa mishipa
mkubwa wa moyo, wagonjwa wengine 13 wamepandikizwa mishipa iliyokuwa imeziba
katika moyo (bypass) isiyopungua miwili.
“Wagonjwa
tuliowapandiza mishipa niwale ambao walikuwa na mishipa zaidi ya miwili
iliyoziba lakini pia kiwango cha ufanyaji kazi wa mioyo yao kilikuwa kimeshuka
sana”,
“Tofauti
ya mishipa hii tunayopandikiza na ile amboyo tumekuwa tukipandikiza siku zote
ni kuwa wagonjwa wengi waliofanyiwa katika kambi hii wana kiwango kidogo cha
ufanyaji kazi wa moyo yaani chini ya 35 (ejection fraction)” alisema Dkt.
Angela
“Kama
Taasisi tumeshaanza kidogo kidogo kufanya upasuaji wa kupandikiza mishipa kwa
wagonjwa lakini tunapokutana na wagonjwa ambao mioyo yao imechoka sana
tunahitaji utaalam zaidi wa kufanya upasuaji bila kuusimamisha moyo na ndio
maana tumekuwa na kambi hii kwa ajili ya kupata mafunzo zaidi na kutoa huduma
kwa wagonjwa wanaohitaji upasuaji wa kupandikiza mishipa.
“Naamini
baada ya kambi hii madaktari wazawa wataweza kufanya upasuaji huu kwa wagonjwa
ambao mioyo yao ina kiwango kidogo cha kufanya kazi chini ya 35 kwani hapo
awali tulilazimika kuwafanyia kwa kusimamisha moyo au kuwatuma wagonjwa hao nje
ya nchi” alisema Dkt. Angela
Kwa
upande wake Daktari kutoka Hospitali ya Max iliyopo nchini India SubhashSinha
amesema kuwa hii ni mara yake ya tatu kufika na kushirikiana na madaktari wa
JKCI kwa sababu maalum za kusaidia kuwafanyia upasuaji wagonjwa ambao mioyo yao
inafanya kazi kwa kiwango kidogo yaani chini ya 35.
“Kila
ninapokuja tumekua tukifanya upasuaji kwa wagonjwa kati ya 20 hadi 25 na wakati
huu tumeweza kuwafanyia upasuaji wagonjwa 20 ambao walikua katika hali mbalimbali
kutokana na mioyo yao kufanya kazi kwa kiwango cha chini”,
“Idara
ya upasuaji ya JKCI inakua kwa kasi katika kutoa huduma za upasuaji, Madaktari
wanajituma sana katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku na wamekua wepesi
kupokea mbinu mpya tunazotumia katika upasuaji kila ninapokuja”, alisema Dkt.
Sinha
Naye
Mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji mkubwa wa kufungua kifua katika kambi hiyo
Abdalla Bakari Mkazi wa Dar es Salaam ameishukuru serikali ya awamu ya nne ya
Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuwa na wazo la kanzisha Taasisi ya Moyo hapa
nchini ili kuweza kuwahudumia watanzania ambao wengi wao hawana uwezo wa
kufuata matibabu ya moyo nje ya nchi.
“Nashindwa
kuongea na haya machozi ninayoyatoa ni ya furaha baada ya kuona tatizo langu la
mishipa ya damu iliyokua imeziba na kunipa changamoto za kuchoka mara kwa mara
na kukosa pumzi wakati nikiwa naongea sasa limetatuliwa, Nawashukuru sana
wataalam hawa waliojitoa kuokoa maisha yetu”,
Comments
Post a Comment