SERIKALI YAHAMASISHA UWEPO WA MAZINGIRA SALAMA NA YENYE KULINDA AFYA ZA WATU MAHALI PA KAZI

 


NA MWANDISHI WETU.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe.Prof. Joyce Ndalichako (Mb) amezungumza na vyomba vya habari kuelekea siku ya kilele cha maadhimisho ya usalama na afya mahali pa kazi na kusema kwamba lengo kubwa la maadhimisho hayo ni kuendeleza kampeni za kuhamasisha uwepo wa mazingira salama na yenye kulinda afya za watu mahala pa kazi.

Prof. Ndalichako ameyaeleza hayo  leo tarehe 27 Aprili, 2022 wakati wa mkutano na wandishi wa Habari kuhusu kilele cha maadhisho ya usalama na afya mahali pa kazi, Jijini Dodoma. Aidha, amefafanua kuwa takwimu zilizotolewa na Shirika la Kazi Duniani kwa mwaka huu zinaainisha kuwa inakadiriwa zaidi ya watu milioni mbili na laki tisa (2.9 milioni) hupoteza Maisha kutokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.

“Kupitia takwimu hizo tunaweza kupata picha na uzito wa changamoto ya madhara yanayo sababishwa na mazingira ya kazi yasiyo rafiki kwa wafanyakazi na ndio maana mwaka huu Shirika la Kazi Duniani limeamua kaulimbiu kuwa ni : kwa pamoja tushirikiane kujenga utamaduni bora wa usalama na afya mahali pa kazi “  alisema Prof. Ndalichako.

Aidha alibainisha kuwa kwa hapa nchini tulianza kuadhimisha siku hii tangu mwaka 2004 ambapo maadhimisho hayo yamekuwa yakiratibiwa na Serikali kupitia Taasisi yake ya OSHA kwa kushirikiana na Wadau wa Utatu ambapo ni Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi- TUCTA na Chama cha Waajiri Tanzania- ATE pamoja na Shirika la Kazi Duniani-ILO. Vilevile Alisema kuwa kwa mwaka huu maadhimisho hayo yatafanyika Jijini Dodoma.

Aidha alisema kama Nchi inashiriki katika kampeni ya kidunia kwa kufanya mambo mbalimbali yanayolenga kukuza uelewa wa masuala ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi na kuhamasisha watanzania kujenga utamaduni bora wa Usalama na Afya katika shughuli za kiuchumi za kila siku.

MWISHO:

 

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.