Na Rhoda Simba, Dodoma.
WAZIRI wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda amesema
kuna umuhimu wa kuangalia upya namna bora ya kupeleka mikopo katika elimu ya
ufundi angalau kwenye ngazi ya stashahada kwa vyuo vya ufundi na ujuzi.
Prof mkenda ameyasema
hayo leo jijini Dodoma wakati akizungumza na bodi ya mikopo (HELSB) ambapo
amesema kuwa waombaji wengi hukosa mikopo wanayoomba kutokana na kutofuata
maelekezo pamoja na kutoambatanisha taarifa zote zinazomhusu muombaji.
Amesema taaluma za ujuzi ndizo zinazohitajika kwenye ajira kwani kilio cha watu wengi ni ajira na sehemu yenye ajira zaidi ni sehemu ya ujuzi na ufundi.
"Mwaka mpya wa
fedha ujao sio Mwaka huu tutapeleka fedha kwa ajili ya wanafunzi wa ufundi
kuweza kupata mikopo"amesema Mkenda
Katika hatua nyingine
amesema ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali CAG Charles Kichere
aliyoitoa hivi karibuni ilieleza kuna shida katika bodi ya mikopo hasa katika
zoezi zima la ugawaji wa mkopo ni kutokana na wanafunzi wenyewe kuandika taarifa
zisizosahihi na wengine kuchelewa kuomba mkopo.
Amesema wamezungumza
na bodi na wamepata taarifa kuwa tatizo lilikuwepo huko nyuma na sasa kuna
maboresho makubwa mpaka sasa na juhudi za kuboresha zitaendelea .
"Kwa sababu mkopo
unatolewa kwa taarifa zinavyotolewa na wanafunzi wanaomba mkopo hivyo
mwanafunzi akichelewa au ukitoa taarifa sio kamili anaweza kukosa mkopo ingawa
una vigezo vya kupata mikopo," amesema
Na
kuendelea"tumekubaliana na bodi ya mikopo tunaendelea kuchakata na kila mtu
ambaye CAG ameona amekosa mkopo na aliyestahili kupata mkopo kuwe na taarifa
itakayokwenda bungeni na kukukutana na kamati ya bunge na hapo kutakuwa na fursa
ya kuhabarisha Umma zaidi," amesema.
Hata hivyo amesema ukaguzi huo ulifanyika kama miaka miwili iliyopita na maboresho yamefanyika na
maboresho yanaendelea ili kuhakikisha wale wote wanafunzi wanaostahili kupata
mkopo waweze kupata mkopo.
Pia Prof. Mkenda ametoa
wito kwa wanafunzi wanaomba mkopo pindi wanapoomba mikopo kuandika taarifa
iliyosahihi na kusema kuwa ukikosea kitu kimoja na bila ushahidi unaweza kukosa na
wanapokwama watoe taarifa kwa bodi ya mikopo na bodi imesema watajitahidi
kushughulikia kwa haraka.
Aidha,prof mkenda
amesema Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imetenga bajeti kwajili ya wanafunzi
wanaofanya vizuri upande wa sayansi watapata udhamini wa masomo(scholarship)
huku akiyataka makapuni mbalimbali nchini kutoa fursa kwa wanafunzi ili kuwatia
moyo wasome kwa bidii na kupata ufaulu mzuri.
Kwa upande wake Prof.Hamisi Dihenga Mwenyekiti wa bodi ya mikopo (HELSB) amesema wao kama bodi watahakikisha kwamba utaratibu wa kutoa mikopo ni utaratibu unao eleweka pamoja
na kuhakikisha mikopo wanayotoa inawalenga wale wanaostahili kupewa.
MWISHO.
Comments
Post a Comment