MKOA WA RUVUMA WAADHIMISHA MUUNGANO KWA KUFANYA USAFI

 



MKOA wa Ruvuma umeadhimisha miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na

Zanzibar kwa kufanya mazoezi na usafi wa mazingira katika Wilaya zote.

Akizungumza kwenye viwanja vya Soko Kuu la Songea,baada ya kukamilika kwa

zoezi la usafi Manispaa ya Songea,Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma

Mhe. Pololet Mgema aliwataja waasisi wa Muungano kuwa walipigania Uhuru wa

nchi yetu na kufanikiwa kuunganisha nchi mbili kuwa Jamhuri ya Muungano wa

Tanzania.

”Muungano wetu umedumu kwa miaka 58,na umeendelea kuimarika,amani na

umoja tulionao leo watanzania ni matunda ya waasisi wa Taifa letu

tunawashukuru sana ’’,Alisisitiza Mkuu wa Mkoa.

Maadhimisho hayo yaliaanza saa 12:30 Asubuhi kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa

kwa kuanza na mazoezi ya kukimbia kuelekea katika maeneo ya kufanya usafi

katika masoko mawili ya Manzese na Soko kuu la Halmashauri ya Manispaa ya

Songea.

Akizungumzia usafi wa mazingira,Mkuu wa Mkoa amewataka wananchi

kuendelea kufuata utamaduni wa kufanya usafi katika maeneo wanayoishi na

wanayofanyia biashara na kwamba usafi ni ishara ya tabia njema kuufanya mji wa

Songea kupendeza.

“Sisi wanaruvuma tulikwishajiwekea utamaduni wa kufanya usafi siku zote katika

maeneo yetu, na maeneo ya umma lakini Ndugu zangu siku za karibuni utamaduni

huo umeanza kufifia ndio maana tukasema tutumie siku ya leo kukumbushana

wajibu wakufanya usafi”, alisisitiza.

Hata hivyo Mkuu wa Mkoa amewahimiza wananchi kufanya usafi kila siku ili

kuepuka magonjwa yatokanayo na uchafu na kwamba gharama za matibabu ziko

juu hivyo ni vyema kujijengea tabia ya kufanya usafi maeneo ya kuishi na maeneo

ya kazi ili kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya kuambukiza.

Pia amesisitiza kufanya mazoezi ya viungo kila Jumamosi ili kuendelea kulinda

afya na kupunguza magonjwa yasiyoambukiza kila kisukari na shinikizo la damu.


Awali Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Ndugu Stephen Ndaki akizungumza

kwenye maadhimisho hayo alisema kila mwaka Siku ya Muungano imekuwa

ikiadhimishwa kwa kufanya shughuli mbalimbali ambapo mwaka huu katika

Mkoa wa Ruvuma siku hiyo imeadhimishwa kwa kufanya usafi wa mazingira na

mazoezi.

Amesisitiza wananchi kuendelea kufanya usafi wa mazingira kila siku badala ya

kusubiri Siku ya Muungano ambapo amesema katika masoko ya Manispaa ya

Songea hali ya usafi hairidhishi hivyo ameagiza wananchi wote kufanya usafi.

Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Philipo Beno alisema

uzalishaji wa taka katika Manispaa ya Songea umeongezeka na unakadiriwa

kufikia tani 80 kwa siku wakati uwezo wa Halmashauri kuzoa taka ni tani kati ya

50 hadi 60 kwa siku.

Hata hivyo amesema Manispaa ya Songea imejipanga na kuweka mikakati ya

kuhakikisha taka zote zinazolewa kila siku kwa kuongeza magari ya kuzolea taka

na kuanzisha kampuni binafsi ya kuzoa taka.

Maadhimisho ya Muungano yametimiza miaka 58 toka kuunganishwa kwa nchi

mbili kati ya Tanganyika na Zanzibar chini ya waasisi Mwl. Julius Nyerere na

Sheikh Abeid Amani Karume.

Imeandaliwa na Albano Midelo

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.