Na Munir Shemweta, WANMM ARUSHA
Serikali imekabidhiwa mashamba yaliyokuwa
yakimilikiwa na Kampuni ya Tanzania Plantations Ltd yenye ukubwa wa ekari
6,176.5 katika wilaya za Arusha na Arumeru mkoani Arusha na hivyo kumaliza
mgogoro wa muda mrefu.
![]() |
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikuzungumza wakati wa makabidhiano ya mashamba ya Tanzania Plantations Litd na Serikali wilayani Arumeru mkoani Arusha |
Mgogoro kati ya Kampuni ya Tanzania Plantations Ltd
na Serikali uliibuka mwaka 1999 baada ya kampuni hiyo kupinga ubatilisho wa
mashamba yake uliofanywa na serikali kutokana na kampuni hiyo kushindwa
kutimiza masharti ya umiliki jambo lililoifanya kufungua kesi Mahakama Kuu
Kanda ya Arusha mwaka 2015.
Hata hivyo, katika kutafuta suluhu nje ya Mahakama
Serikali kupitia Wakili Mkuu wa Serikali Mei 15, 2019 aliwasilisha ombi la
kufanya majadiliano na mdai kwa lengo la kumaliza shauri nje ya mahakama ambapo
Mahakama iliridhia pande mbili za shauri kumaliza suala hilo nje ya mahakama.
Makabidhiano ya mashamba hayo yaliyokuwa
yakijulikana kama Karangai na Lucy Estate yanahitimisha mgogoro kati ya
serikali na Kampuni ya Tanzania Plantations Ltd sambamba na ule wa wananchi
uliotokana na wananchi kuuziwa baadhi ya maeneo kwenye mashamba
yaliyobatilishwa.
Katika makubaliano ya kutafuta suluhu nje ya
mahakama, Serikali ilikubali kulipa shilingi bilioni 5.7 kwa ajili ya fidia ya
mashamba Na 304 na 305 Nduruma yenye ukubwa wa ekari 6,133 na shamba la
ekari 43.5 ambalo halikubatilishwa lakini ilionekana ni busara likachukuliwa na
serikali. Pia serikali ililipa fidia ya mkonge na mtambo wa kuchakata mkonge
uliokuwa ukifanya kazi.
Makabidhiano ya mashamba hayo yalifanyika jana
tarehe 29 April 2022 katika kata ya Bwawani wilayani Arumeru mkoani Arusha
baina ya Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Allan
Kijazi na Mkurugenzi wa Tanzania Plantation Ltd Bw. Ladhia Prabhudas Pradip
mbele ya Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mashamba
hayo, Waziri wa Ardhi, Dkt Angeline Mabula alisema, Mhe Rais aliridhia
makubaliano yafanyike na kutoa fedha kwa ajili ya fidia kumaliza mgogori huo
uliodumu kwa muda mrefu.
"Tunamshukuru sana Mhe Rais, Samia Suluhu
Hassan kwa sababu masuala haya yanahitaji hekima na busara na aliliona hili
kuwa kuna uhitaji wa kuwa na mazungumzo na Tanzania Plantation Ltd lakini pia
akiangalia mustakabali wa watu waliokuwa eneo, tunamalizaje hili na kuelekeza
makubaliano yafanyike na akatoa fedha na tayari mmiliki alishalipwa"
alisema Dkt. Mabula
Kwa mujibu wa Dkt. Mabula, Serikali ya Mama Samia
haiwezi kuwatelekeza wananchi waliokuwa wakiishi katika mashamba hayo na
kubainisha kuwa itaweka utaratibu mzuri ili wananchi hao waweze kufaidika na
matunda amabayo serikali imepanga.
Ametoa agizo kwa halmashauri ambazo ni mamlaka za
upangaji nchini kuendelea kufanya tathmini kwa yale mashamba ambayo wamiliki
wake wameshindwa kuyaendeleza au kuyatelekeza hatua za kuyatwaa uanze kufanyika
mara moja.
Kwa upande wake Katibu Mkuu, Wizara ya Ardhi Nyumba
na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Allan Kijazi alisema, Wizara yake kwa kushirikiana
na wizara na taasisi nyingine imeanza kuchukua hatua zitakazoiwezesha serikali
kufanya maamuzi kuhusu matumizi ya mashamba hayo ikiwemo uvunaji wa
mkonge kwa kuzingatia baadhi ya mahitaji ya wananchi .
"Serikali imeweka pia utaratibu wa ulinzi wa
mashamba sambamba na mamlaka ya mkoa kusimamia mali kipindi hiki ambacho
mpango wa matumizi ya ardhi unaandaliwa na niwatake wananchi kutoa
ushirikiano" alisema Dkt Kijazi
![]() |
Mkuu wa mkoa wa Arusha John Mongela akikuzungumza wakati wa makabidhiano ya mashamba ya Tanzania Plantations Litd na Serikali wilayani Arumeru mkoani Arusha |
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela
aliwatahadharisha wananchi wa eneo hilo kuwa eneo hilo sasa ni mali ya
serikali na wanachotakiwa ni kusubiri utaratibu wa matumizi ya mashamba hayo
utakapowekwa.
"Asitokee mwananchi kufanya eneo hili kuwa
shamba la bibi na mara kadhaa vinara namba moja katika kuanzisha migogoro ni
viongozi hivyo niwatake viongozi wa vijiji na vitongoji msiwe madalali na
tusije tukalaumiana, wajibu wa viongozi ni kusimamia wananchi na mali zao
na kutaka wasianzishe migogoro.
Naye Kamishna wa Ardhi nchini Nathaniel Methew
Nhonge alisema, baada ya makabidhiano ya shamba yaliyofanyika sasa ni lazina
eneo hilo liandaliwe mpango wa matumizi ya ardhi kwa ajili ya manufaa ya nchi na
kusisitiza kuwa zile changamoto zitakazojitokeza zitafanyiwa kazi na kutafutiwa
ufumbuzi .
MWISHO
Comments
Post a Comment