WAZIRI NDALICHAKO ATAKA MUONGOZO WA SADC WA KULINDA AJIRA KWA WATOTO KUZINGATIA MAADILI YA KIAFRIKA

Na. Lusajo Mwakabuku, OWM-KVAU Dodoma.

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce L. Ndalichako amewataka wajumbe wa mkutano wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuhakikisha katika mwongozo wa kulinda na kuzuia ajira mbaya kwa watoto ni vyema maneno yaliyotumika yakapatiwa tafsiri ili yaendane na maadili, utamaduni, na mazingira ya kiafrika.

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce L. Ndalichako

Waziri Ndalichako alitoa kauli hiyo mapema leo 30/03/2022 jijini Lilongwe Malawi alipokuwa akishiriki Mkutano wa Mawaziri wa Kazi na Ajira wa SADC waliokutana kujadili mambo mbalimbali juu ya sekta ya Kazi na Ajira ambapo katika kikao hicho ajenda 13 zinazohusu kuweka miongozo mbalimbali ya kusimamia masuala ya ukuzaji wa fursa za ajira, usimamizi wa viwango vya kazi, hifadhi ya jamii na usalama na afya mahala pa kazi.

 

Akitoa mchango wake, Profesa Ndalichako alisema suala la biashara ya ngono kwa mila na desturi ya nchi zetu za Afrika ni suala lisilokubalika, hivyo alisisitiza katika mwongozo huo isitafsiriwe kuwa biashara hiyo inakubalika kwa wasio watoto peke yake kwani kwa mazingira na tamaduni zetu za kiafrika biashara hiyo ni haramu.

 

Masuala mengine yaliyojadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na kupitia rasimu ya Itifaki ya SADC ya Kazi na Ajira, Mwongozo wa kuanzisha Taasisi za Majadiliano ya Waajiri na Waajiriwa, Zana za Ufuatiliaji na Utoaji taarifa kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Uhamaji Nguvukazi ndani ya SADC pamoja na kuanzisha mfumo wa taarifa za soko la ajira wa SADC.

 

Pia mijadala mingine ilifanyika juu ya Hali ya Utekelezaji na Uridhiaji wa Itifaki na Mikataba ya Shirika la Kazi Duniani na pia mkutano huu ulipokea taarifa kuhusu maandalizi ya ushiriki wa nchi za SADC katika Mkutano Mkuu wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) unaotaratijwa kufanyika Mwezi Juni, 2022.

 

MWISHO

 

Comments

Dodoma News
Mwanza City, Mwanza, Tanzania
Dennis G. Harrison, mmiliki mwenza wa Mtandao wa Dodoma News Blog, alizaliwa mkoani Morogoro zaidi ya miaka 40 iliyopita. Dennis ana Taaluma ya Uandishi wa Habari (Proffessional Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT). Mwaka 2009 alimaliza Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma, ikijikita katika Menejimenti ya Uhusiano kwa Umma na Matangazo katika chuo cha SAUT. Mwaka 2002, Dennis aliajiriwa katika Shirika la Posta Tanzania, Ofisi kuu ya Mwanza. Mwaka 2009 aliajiriwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa nafasi ya Afisa Habari. Akiwa katika ofisi hiyo alifanya kazi kwa juhudu na maarifa na kufanikiwa kuchaguliwa na wafanyakazi wote kuwa mfanya kazi bora. Kufuatia juhudi na utendaji kazi wake, alipanda hadi nafasi ya Afisa Habari Mwandamizi.