Na Mwandishi Wetu - Dodoma
Serikali imesema inatarajia kuwajengea uwezo
waraibu wa dawa za kulevya waliopata nafuu kwa kuwapatia mafunzo ya kukuza
ujuzi kupitia vyuo vya ufundi katika fani mbalimbali ili kujiajiri na kuendelea
kufanya shughuli za kiuchumi kuinua kipato chao na kuchangia pato la Taifa.
Hayo yamesemwa Machi 30, 2022 na Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. Balozi.
Dkt. Pindi Chana wakati akiwasilisha taarifa kuhusu utekelezaji wa bajeti ya
mwaka 2021/22 na makadirio ya bajeti ya mwaka 2022/23 kwa Fungu 91 ya Mamlaka
ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na Fungu 92 ya Tume ya
Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Masuala ya UKIMWI na Dawa za Kulevya katika Ukumbi wa Bunge Jijini Dodoma
iliyokutana kujadili na kupitisha bajeti ya Taasisi hizo.
Mhe. Pindi alisema Serikali kupitia Mfuko wa Dunia
wa Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund) imepata fedha
kiasi cha shilingi billioni 2.4 kwa ajili ya kujenga vituo vitatu (3) vya
Serikali vya kutolea huduma za utengamao kwa Waraibu wa dawa za kulevya. Vituo
hivi vitajengwa katika Mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam na Tanga.
“Katika mwaka wa fedha 2021/22 Serikali imeanzisha
Kliniki moja ya Methadone katika Mkoa wa Arusha na ndogo nne katika Mkoa wa Dar
es Salaam na kufanya jumla ya Kliniki zilizopo kuwa 15 ambazo zinatoa matibabu
kwa waathirika wa dawa za kulevya nchini na Ofisi tatu za Mamlaka katika Mikoa
ya Dodoma, Mtwara na Mwanza hivyo kupitia programu hii ya kukuza ujuzi
wanufaika wa mafunzo hayo watapatiwa zana za kufanyia kazi,”Alisema Mhe. Pindi.
Pia Mhe. Waziri Pindi alifafaua kuwa Serikali
inaendelea kufanya Uraghibishi kwa makundi mbalimbali ya kijamii wakiwemo
Viongozi wa Kijamii, Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Viongozi wa Dini, Wanafunzi
wa shule, Vyuo pamoja na jamii kwa ujumla ili kuimarisha mapambano dhidi ya
dawa za kulevya.
“Serikali imezitambua na kuzijengea uwezo Asasi za
Kiraia 77 kwenye Mikoa 18 Nchini. Asasi hizi zinafanya kazi ya kuwafuatilia
waraibu na kuwaunganisha na vituo vya tiba katika kufikia malengo
yaliyokusudiwa ya mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya ambazo matumizi yake
yamekuewa yakiathiri afya za watumiaji na kuharibu nguvu kazi ya Taifa” alieleza Mhe.
Pindi.
Kwa upande wake Kamishna wa Kinga na Tiba kutoka
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Dkt. Peter
Mfisi akijibu hoja za wajumbe wa kamati hiyo alieleza kwamba mamlaka itaendelea
kufuatilia matumizi ya vilevi watashirikiana na mamlaka zinazohusika ili kuhakikisha
wazalishaji wanazingatia afya za watumiaji huku akihimiza waraibu wa dawa hizo
kujitokeza kupata matibabu waweze kurejea katika hali ya kawiada.
“Sisi tunao mpango wa kujenga Kliniki katika Mkoa
wa Shinyanga na mara nyingi tunapojenga tunafanya utafiti kwanza wa ukubwa wa
tatizo katika eneo husika na hizi Kliniki za Methedone zinatibu tu
waraibu wa Heroin kwa kweli tunafanya kila jitihada kuhakikisha mapambano haya
yanafanikiwa,”alisisitiza Dkt. Mfisi.
Kuhusu Masuala ya UKIMWI Mhe. Pindi alibainisha
kwamba Serikali inatekeleza Kampeni ya FURAHA YANGU inayolenga kuhamasisha
upimaji wa VVU kwa wanaume ambapo imesaidia kuongezeka kwa idadi ya watu
wanaopima VVU kutoka asilimia 61 mwaka 2016 hadi asilimia 81 mwaka 2020 wakati
lengo ilikiwa ni kufikia asilimia 95 ifikapo mwaka 2023.
“Serikali inashirikiana na Asasi zisizo za
kiserikali na wadau mbalimbali katika upimaji na tohara kwa wanaume kupitia
Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI wa mwaka 2018/19-2022/23,” alifafanua
Mhe. Pindi.
Vilevile, Mhe. Pindi alisisitiza kwamba elimu ya lishe
imetolewa kwa Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (WAVIU) katika Konga 180
kupitia Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA) kwa kuzingatia
makundi 5 ya vyakula ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha kulima mazao yanayoweza
kuwapatia chakula bora.
Aidha, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala
ya UKIMWI na Dawa za Kulevya, Mhe. Fatma Taufiq alieleza kwamba baada ya wajumbe
kujadili bajeti ya taasisi hizo imepitisha kwa kauli moja Makadirio ya bajeti
ya mwaka wa fedha 2022/23 kwa fungu 91 ya mamlaka ya kudhibiti na kupambana na
dawa za kulevya na fungu 92 ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania kiasi cha
shilingi Bilioni 26.9.
MWISHO
Comments
Post a Comment